24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

ACT-Wazalendo yalilia maisha ya Wazanzibari

ZittoNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar, imeelezwa kuathiri maisha ya wananchi huku bei za vyakula ikipanda kwa kasi na kufikia asilimia 16 hadi 30.

Licha ya hali hiyo pia mfumko wa bei  umepaa na kufikia asilimia 11,  tofauti na miaka ya hivi karibuni.

Taarifa iliyotolewa jana na Kiongozi  wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe,  ilieleza kuwa sekta ya utalii ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar imeathirika kiasi kikubwa, ambapo hivi sasa hoteli  zimekuwa zikipokea nusu ya idadi ya watalii waliotarajiwa kipindi cha mwishoni mwa mwaka.

Alisema kupitia taarifa hiyo kuwa athari hiyo  ya kutokuja kwa watalii haiwagusi wamiliki wa hoteli pekee, kwani ujio wa wageni husaidia kuchagiza biashara mbalimbali za wenyeji zikiwamo za waongoza watalii, wauza bidhaa pendwa, wasafirishaji na kada nyingine katika mnyororo wa biashara ya utalii.

“Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar, mfumko wa bei wa Zanzibar, hivi sasa umefikia kiwango cha asilimia 11 ambacho hakijawahi kufikiwa katika miaka ya karibuni.

“Bei za bidhaa hususani vyakula zimepanda kwa kiwango cha asilimia 16.4, huku vyakula vya baharini, mfumuko wake wa bei umefikia asilimia 30. Kwa kulinganisha, mfumuko wa bei kwa Tanzania ni asilimia 6.6 kwa mujibu wa taarifa ya mwezi uliopita ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

“Huu ni ushahidi wa wazi kwamba mkwamo huu wa kisiasa umeanza kuwaumiza wananchi wasio na hatia. ACT inasikitishwa na hali ngumu ya maisha inayowakumba wananchi wa Zanzibar kutokana na mkwamo wa kisiasa,” alisema Zitto.

Alisema wakati wa mkutano wa chama hicho wa tathmini ya hali ya kisiasa ya Zanzibar uliofanyika mjini Unguja Desemba 19 na 20, mwaka huu,  viongozi wa ACT-Wazalendo walipokea taarifa kutoka kwa wananchi wa kawaida kuhusu nini hasa kinaendelea.

“ACT-Wazalendo inasema kwamba hali hii ya kuumiza wananchi wa kawaida haikubaliki na ni lazima ifikie ukomo haraka iwezekanavyo. Hatuwezi kuumiza wananchi wetu kwa sababu zisizo na maana,” alisema.

Chama hicho kinataka mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu atangazwe haraka ili hali ya utulivu wa kawaida irejee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles