WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewaonya watendaji wa halmashauri nchini ambao watabainika kutumia vibaya fedha za Serikali na kusema kuwa watang’olewa kazini.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Ilulu.
“Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu, ole wake. Yeyote atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng’oa. Wako wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira.
“Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza kujali wananchi. Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, ” alisema.
Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi jana mkoani hapa aliwaeleza wakazi hao kwamba amekwenda kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao ambapo aliahidi kutomwangusha Rais John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa nafasi ya uwaziri mkuu.