WIKI mbili zilizotangulia wiki iliyopita niliandika kuhusu Bunge na utendaji wake. Makala ya kwanza kati ya hizo ilihusu hatua ya Bunge kukataza matangazo ya moja kwa moja ya vikao vyake.
Hatua hiyo imezua majadiliano makubwa katika jamii ambayo kimsingi hayana tija yoyote. Majadiliano hayo hayana tija kwa sababu yanajikita katika suala ambalo mtu mwingine akilisikia atakachokifanya ni kutuhurumia. Atatuhurumia kwa sababu wakati jamii nyingine zikijitahidi kujikita kuendana na wakati, hasa katika suala la uwazi, sisi tunajirudisha nyuma. Badala ya kukumbatia usasa, sisi tunakimbilia ujima!
Wakati wengine wakifikiria jinsi ambavyo wanaweza kutumia kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano kama njia ya kuleta maendeleo, sisi tunafikiria jinsi ya kupambana na teknolojia!
Ni aibu kulumbana kuhusu kuonyesha au kutoonyesha moja kwa moja vikao vya Bunge wakati huo huo tukijigamba ni nchi ya kidemokrasia ambayo inaheshimu na kuthamini haki za binadamu. Ni aibu kujadili mambo hayo katika mazingira ambayo wahusika wanatoa sababu za ajabu wakitafuta kuhalalisha hatua zao za kuchekesha za kukatisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.
Makala ya pili niliiandika nikiwasihi wabunge kuacha siasa wakati wa kujadili bajeti. Niliandika makala hiyo nikiwa nimeanza kuhisi kitakachotoka bungeni hasa baada ya mjadala wa kukatisha matangazo ya moja kwa moja kushika kasi. Katika makala hiyo niliwasihi wabunge kuwa wanapoingia kwenye hatua hii muhimu ya kujadili jinsi nchi itakavyoendeshwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, waache tofauti zao za kisiasa na kujikita katika mjadala ambao utajali maslahi ya nchi na wananchi.
Lakini kinachotokea bungeni kinaashiria kile kile ambacho nilikihisi kiasi cha kuwakumbusha wabunge kuwa wanachokwenda kukifanya bungeni katika miezi hii miwili hakipaswi kuwa sehemu ya propaganda zao za kisiasa.
Wabunge wanapaswa kufahamu kuwa maisha ya Watanzania wote kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao yapo chini ya uangalizi wao. Kile wanachokifanya ndicho kitakachotengeneza mustakabali wa Watanzania. Kama wakifanya kazi ya maana, watasaidia sana kuboresha maisha ya Watanzania.
Lakini kwa upande wa pili wakijikita katika maslahi ya kwao binafsi na vyama vyao, basi watawaumiza mamilioni ya Watanzania ambao wamewaamini na kuwapa nafasi hiyo.
Ni jambo la bahati mbaya sana kuwa yale niliyohisi yatatokea yanatokea kweli. Ingawa matangazo ya Bunge hayarushwi moja kwa moja lakini baada ya wiki tatu, taarifa zinaonyesha kuwa majadiliano bungeni yametawaliwa na siasa zaidi kuliko kujadili hoja zinazohusu bajeti zinazowasilishwa. Taarifa zinaonyesha kuwa lugha chafu, za kashfa na matusi ndizo zinazotawala katika mijadala bungeni. Kwa dalili zilizopo, inaonekana kuna udhaifu wa aina fulani katika kuwadhibiti wabunge katika mijadala. Ni kukosekana huko kwa udhibiti ndiko kunafanya mijadala inayotawaliwa na lugha za matusi na kashfa kutamalaki bungeni.
Kama kungekuwa na udhibiti wa kutosha dhidi ya wabunge wanaotumia lugha za aina hiyo, naamini kuwa isingefikia mahali baadhi ya wabunge wangefikia hatua ya kususia kikao baada ya hoja yao ya kutaka mwenzao aliyetumia lugha ya kuudhi dhidi yao adhibitiwe. Naamini kuwa iwapo uongozi ungekuwa makini na kumdhibiti aliyetoa lugha ya kashfa na matusi, basi wabunge hawa waliosusia kikao wangeendelea kutoa mchango wao.
Lakini kwa upande mwingine, sakata hilo la baadhi ya wabunge kususia vikao linaonyesha sura ya kisiasa zaidi kwa sababu waliosusia ni wa upande mmoja. Hii inatoa sura kuwa pamoja na kuwa kinacholalamikiwa kinaweza kuwa na mashiko, lakini suala hilo limechukua mrengo wa kisiasa. Si ajabu kuwa pengine hata udhibiti wa wabunge wanaokwenda kinyume na kanuni za Bunge unakuwa mgumu kwa sababu za kisiasa.
Dhamira ya kuwasihi wabunge wazingatie maslahi ya umma watakapokuwa wanajadili bajeti inatokana na ukweli kufanya hivyo kungezidisha umoja na mshikamano wa Watanzania. Kama wabunge wangeweza kuweka tofauti zao za kiitikadi pembeni na kuijadili bajeti kwa maslahi ya Taifa, kungetoa taswira ya umoja na mshikamano.
Kama hilo lingefanikiwa na kuwezesha upitishwaji wa bajeti inayoakisi maslahi ya Mtanzania, picha hiyo ingeweza kuwa chachu ya kuwaunganisha Watanzania katika masuala mbalimbali. Lakini hivi sasa tunashuhudia makundi ya wabunge yakitoka nje ya vikao baada ya kushindwa kuelewana na wenzao ndani ya Bunge. Sijui kama Bunge linaelewa fika maana ya hatua hii ya makundi kutoka bungeni baada ya kushindwa kuelewana kwenye vikao vyao vya ndani. Lakini majuzi tulishuhudia hilo likienda mbali zaidi. Wabunge wanawake kutoka kambi ya upinzani walieleza kuwa wameuandikia uongozi barua ya kujitoa katika Umoja wa Wabunge Wanawake. Hili linapaswa kuwa jambo la kushitua sana.
Kama nilivyobainisha hapo juu, wabunge wanapokuwa kazini wanapaswa kufanya kazi kama kitu kimoja na kujenga umoja na mshikamano. Sasa tunaposhuhudia baadhi ya wabunge wakijitoa katika taasisi za kibunge ambazo zinalenga kuwaleta pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano wao, picha inayojengeka ni mfarakano.
Ni matarajio yangu kuwa uongozi wa Bunge utalichukulia kwa umakini mkubwa na kulifanyia kazi haraka suala hili la baadhi ya wabunge kuonyesha dhamira ya kujitoa katika umoja wao. Sidhani kama uongozi wa Bunge unafurahishwa kuona kuwa badala ya kuungana, wabunge wanazidi kufarakana.
Ingawa suala hili limechukua suara ya kisiasa, haifai kwa uongozi wa Bunge nao kulichukulia kuwa ni suala la kisiasa. Uongozi wa Bunge unapaswa kuchukua nafasi yake kama mzazi na kuhakikisha kuwa taasisi iliyo chini yake inaimarika badala ya kusambaratika.
Upo uwezekano kuwa kwa kuwa waliotangaza kujitoa ni wapinzani, basi wataachiwa wajitoe kwa sababu watakaobaki watakuwa na uwezo wa kuendelea na shughuli bila kuathirika. Kufanya hivyo urakuwa ni mwendelezo wa kuigawa nchi.
Tulishuhudia katika Bunge la Katiba baada ya wapinzani kususia, wale waliobaki wakiendelea na mijadala lakini matokeo yake yamezaa Rasimu ya Katiba ambayo hata hao waliobaki kujadili wanaamini mioyoni mwao kuwa haisimamii maslahi mapana ya Tanzania.
Hatua kama hizi za kuchukulia kila kitu kisiasa kimeanza kumomonyoa umoja na iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, tusije kumtafuta mchawi tutakapofikia hatua ya kupigana wenyewe kwa wenyewe.