23.4 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

Ama kweli mkuki kwa nguruwe…..

34MISEMO ya Kiswahili mara nyingi hunifanya niwe nawaza na kuona ni jinsi gani wazee wetu walivyokuwa wanafikiria wakati wanaitunga hiyo misemo, unaweza ukaisikia muda mrefu na usione misemo hiyo inatumika wapi ila siku litakapotokea jambo fulani ndio utatambua matumizi yake.

Baada ya kutokea sakata la sukari na kubainika kuwa kuna wafanyabiashara wanaficha sukari na Serikali kujiapiza kuwashughulikia na ndio nikakumbuka tukio la Serikali kuzuia Bunge lisonekane ‘live’ ambapo kwangu mimi matukio haya mawili hayana tofauti sana kwa kuwa hawa wote wanajaribu kuwanyima wananchi haki zao za msingi na ndipo nikakumbuka kumbe mkuki wa kuwanyima wananchi kukosa Bunge hauumi kwa kuwa sisi tumeshazoea kuonewa lakini mkuki wa sukari umekuwa mchungu kwa Serikali kwa kuwa inaonekana kama ni hujuma kwa Serikali iliyo madarakani dhidi ya wananchi wake.

Wanasiasa na wafanyabiashara hawa ni watu wanaofanana japo kila mtu ana eneo lake la kufanya mambo yake, nitajaribu kuelezea ni kwa namna gani watu hawa wanafanana.

Mfanyabiashara mtaji wake ni wananchi ambapo ili biashara iendelee anawahitaji wananchi ambao kiuhalisia ni wateja wake lakini pia katika biashara mfanyabiashara mara nyingi hufikiria ni kwa namna gani atabuni mbinu zake ili aimarishe faida yake na kwa bahati mbaya muda mwingine huwabidi kufanya hata mbinu za kihuni kama hizo za kuficha sukari ili iwe adimu mtaani halafu ukifika muda fulani waiuze kwa bei ambayo itawafanya wapate faida maradufu tofauti na faida ambayo wangeipata hapo awali.

Niliwahi kuzungumza na rafiki yangu mmoja ambaye ana duka linalouza vyakula kipindi kile Bodi ya Sukari ilipoagiza wauzaji wa rejareja kuuza sukari kwa bei elekezi ya Sh.1,800, akaniambia kuwa huu uamuzi wa kisiasa unaofanywa kwa kukurupuka huwa haufai maana wao wauzaji wa rejareja hununua sukari hiyo kwa wauzaji wa jumla ambao wauzaji hao wa jumla huwauzia sukari kwa bei ya Sh.1,940 sasa ni nani ambaye angekubali kuuza sukari kwa bei hiyo elekezi?

Hivi sasa sukari hiyo kwa wauzaji wa rejareja imefika mpaka Sh. 3,000 na maeneo mengine mpaka Sh.3,500. Sasa hivi sukari imekuwa adimu na uadimu huo inafanya wale wauzaji walioficha sukari kufanya biashara ambayo inawapa faida maradufu maana sasa hivi wauzaji wa rejareja wananunua kiroba cha sukari cha kilo 25 kwa shi Sh. 60,000 na kuendelea hii ina maana kilo moja inanunuliwa kwa Sh. 2,400 ambapo yeye huiuza kwa SH. 2,800 na kuendelea sasa kwa mtindo huu ni nani aliye tayari kuuza sukari kwa bei ile elekezi? Sasa wafanyabiashara wakubwa wamejiingiza kati hapo wameamua kuificha hiyo sukari na kufanya lawama za wananchi zielekezwe kwa viongozi ambao kwao wanasiasa wameona kama hizi ni hujuma dhidi ya Serikali yao hivyo wanajaribu kutafuta kila namna ambayo itawafanya washinde vita hii na kurudisha ile imani yao dhidi ya wananchi wasiofurahishwa na mfumuko huu wa bei ya sukari.

Mimi binafsi napongeza hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya mtu yeyote ambaye kwa namna moja au nyingine anajaribu kuongeza gharama za wananchi pasipo na sababu za msingi wowote lakini pia nataka kuwaambia Serikali hili suala la wafanyabiashara kuficha sukari halina tofauti na tukio la Serikali kutufichia Bunge kwa sababu wanazozijua wao wenyewe.

Ukisema kurusha Bunge ni gharama Je, unalinganisha gharama hizo na kitu gani? Kuna vitu ili uvipate inabidi ugharamike maana havina bei chee na wakati Rais anazungumza kuhusu kupunguza matumizi yasiyo na faida sidhani kama Bunge linahusika katika mambo yasiyo na faida. Tulipoamua kuwa nchi yenye demokrasia bila shaka tulikubaliana na gharama zake maana demokrasia ni ghali sio kitu cha bei rahisi, Tunataka Serikali yenye uwazi na uwajibikaji sasa kama mmeanza kuwawajibisha wahujumu uchumi kwa nini msituachie chombo kinachojaribu kuweka mambo wazi? Wafanyabiashara wanaficha sukari mnataka kutuaminisha kuwa wao ni mashetani kwa kuwa tu wanafanya jambo ambalo linaweza kuwaondolea imani hiyo kwa wananchi Je, nyie mnaolificha Bunge nyie ni nani? Ni malaika kwa kuwa mnadai mnapunguza gharama za Serikali kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja? Hoja ya kusema kuwa vyombo haviruhusiwi kuingia bungeni kurusha matangazo mpaka studio ya Bunge itakapotengenezwa ni dhaifu sana, sawa tuseme mlikubaliana hivyo kama alivyosema Waziri mwenye dhamana na habari lakini ndio mlikubaliana kuwa mtaanza ujenzi huku bunge likiwa linaendelea?

Na mkianza mchakato huo vyombo vya habari havitaruhusiwa kurusha Bunge? hii si sawa, ninyi ni kama waficha sukari sema utofauti wenu unakuja pale ambapo mnasikia uchungu juu ya mambo hayo, mmekataa matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja haliwaumi kwa sababu mnaona huo ni mtaji wenu kisiasa kwenye kuwazuia wapinzani ila mnasahau kuwa mnatunyima wananchi haki yetu ya msingi ya kupata habari ambapo hii ni haki kama haki nyingine katika nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, demokrasia ni ghali kama nilivyosema hapo awali ila suala la sukari linawauma kwa sababu mnaona kama hili linawaathiri moja kwa moja maana kama kuna mambo yalifanya Serikali ya Awamu ya Tano ilaumiwe basi ni mfumuko wa bei na mbaya zaidi hili la sukari limekuja baada ya kauli za kuchanganya za viongozi kama ile ya kuzuia sukari kutoka nje ndio maana mmeona kama suala la kuvalia njuga.

Endeleeni kutumbua majipu ya kuficha sukari ila mkimaliza tunawaomba na nyie mjisafishe kwa kuturudishia Bunge maana kuficha sukari hakuna tofauti na kuficha Bunge, nyie wote kuna haki ya msingi mnatunyima. Kama ambavyo mnasikia maumivu tunapolalamika sukari kuwa ghali na kuadimika mtaani ndivyo tunavyoomba mturudishie Bunge ndipo tutawatambua kama Serikali sikivu na sio kushughulikia yale mnayoona yanauma maslahi yenu tu na sisi wananchi mnatuacha tukiendelea kusema pasipo nyie kuchukua uamuzi wowote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles