Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanzisha ushirikiano na taasisi tatu za kimkakati katika juhudi za kuwasaka wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na CREDITINFO Tanzania Ltd, ambayo inahusika na uchakataji wa taarifa za wakopaji katika taasisi za fedha.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo Septemba 11, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, alieleza kuwa lengo kuu la ushirikiano huu ni kuongeza ufanisi wa kuwatambua wadaiwa wa mikopo hasa waliopo kwenye sekta binafsi na isiyo rasmi kwa kutumia mifumo ya TEHAMA iliyounganishwa. Alisema kuwa hili ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuzitaka taasisi za serikali kushirikiana na kubadilishana taarifa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
“Katika kazi yetu ya kukusanya mikopo, tunawahitaji wadau hawa ili tuweze kuwafikia wadaiwa wote kwa kutumia mifumo ya kisasa,” alisema Dk. Kiwia. Aliongeza kuwa HESLB itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuboresha utendaji kazi wake.
Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, alisema kuwa taasisi yake itaendelea kutoa huduma kwa wakati kwa kushirikiana na HESLB. Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Deusdedit Buberwa, alifafanua kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya kutekeleza agizo la Serikali la kuunganisha mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CREDITINFO, Edwin Urasa, alihimiza wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kujitokeza na kuanza kurejesha mikopo yao ili kuimarisha uaminifu wao kwa taasisi za kifedha. “Ni muhimu kwa wakopaji kuanza kurejesha madeni yao, ikiwa ni pamoja na mikopo ya elimu ya juu, ili waweze kuaminika zaidi katika kukopeshwa na taasisi za kifedha,” alisema Urasa.
Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha kuwa wadaiwa wote wanapatikana na kuwajibika katika urejeshaji wa mikopo, hatua inayolenga kuboresha mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.