Nora Damian, Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imewataka wazazi wenye uwezo kuwasomesha watoto wao ili mikopo isaidie watoto wanaotoka katika familia duni.
Aidha, imesema wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaopata mikopo ni zaidi ya 40,000 na wanaoendelea na masomo kwa mwaka wa amasomo 2018/19 ni zaidi ya 80,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 10, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-razaq Badru, amesema Sh bilioni 427 zimetengwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.
“Maombi yataanza kupokelewa kuanzia leo hadi Julai 15 mwaka huu lakini niombe kwa msisitizo wazazi wenye uwezo kusomesha watoto wao ili mikopo iwasaidie wasio na uwezo,” amesema.