MADRID, HISPANIA
NYOTA mpya wa Real Madrid, Eden Hazard, anatarajiwa kutambulishwa leo kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu huku maandalizi yake yakidaiwa kuyafunika yale ya Cristiano Ronaldo wakati anajiunga akitokea Manchester United.
Ronaldo alijiunga na Real Madrid mwaka 2009, ambapo mapokezi yake kwenye uwanja huo yalishuhudiwa na mashabiki 70,000 waliojitokeza uwanjani hapo, lakini hii ya Hazard inadaiwa inaweza kufunika ya Ronaldo.
kwa mujibu wa gazeti la Marca la nchini Hispania, mashabiki wamejipanga kwa wingi kujitokeza uwanjani hapo kwa ajili ya kumpokea mchezaji huyo.
Hazard raia wa nchini Ubelgiji, amesaini kuitumikia Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitano huku uhamisho wake ukitajwa kuwa na thamani ya pauni milioni 150 akitokea timu ya Chelsea.
Hazard ni mchezaji ambaye anatajwa kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika historia ya timu hiyo. Hata hivyo tayari Madrid wamefanya usajili mwingine wakati huu wa kiangazi ikiwa pamoja na Luka Jovic kwa uhamisho wa pauni milioni 62 akitokea timu ya Frankfurt.
Tayari mchezaji huyo ametambulishwa mbele ya mashabiki jana na tayari amerudi katika timu ya taifa ya Serbia kwa ajili ya kwenda kushiriki michuano ya Euro inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 21.