HATUNA budi kuhoji maneno yanayoenea kwa kasi kuwa Profesa Ibrahim Lipumba hataki uenyekiti CUF, na kwamba alikwisha kukitosa chama hicho karibu sana na Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Kwamba anachokitaka ni kuhakikiska kuwa CUF inagawanyika kati ya Tanzania Bara na Visiwani; wakati huku Bara wanachama wanaendelea kusutana, kutukanana, kupigana na kufarakana.
Kwamba pia eti anataka kuvuruga Upinzani nchi nzima, mbali na kuisambaratisha kabisa CUF. Kwamba na hatua ya jeshi la polisi kumsindikiza kurejea ofisini na kuvunja milango ya kuingilia ofisini humo ni kitendo ambacho kinapaswa kutafakariwa, akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa aliyetoa kauli kuwa bado anatambua uenyekiti wake kwa CUF.
Wakati hayo yakitendeka, CUF yenyewe imemshangaa Profesa Lipumba; na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, amesema kuwa hatambui kurejeshwa kwa Profesa Lipumba kuongoza chama hicho.
Profesa Lipumba alijiuzulu mwenyewe uenyekiti mwaka mmoja uliopita wakati Uchaguzi Mkuu unakaribia kwa madai kuwa hakufurahishwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa mgombea wa urais kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama vinne vya Upinzani.
Tangu Baraza Kuu la CUF lililofanyika Agosti 29, mwaka huu, kutangaza kumsimamisha uanachama Profesa Lipumba, yeye amekuwa akiwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha kuwa anakuwa kiongozi wa CUF tena.
Wengine wameuita sinema mtafaruku huu, yaani mchezo wa kuigiza. Wameuita hivyo baada ya Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, ili kumhoji Profesa Lipumba.
Wakati wajumbe wa Baraza hilo wakijiandaa kukutana leo Unguja kutekeleza mpango huo, juzi kutwa nzima, Profesa Lipumba alikuwa na kikao kizito na walinzi wa chama hicho (Blue Guard) makao makuu ya CUF Buguruni, Dar es Salaam.
Wakati huo taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui, ilisema baraza hilo linamtaka Profesa Lipumba afike mbele ya kikao hicho ili ajieleze na kujitetea kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia ofisi za makao makuu na kusababisha uharibifu wa mali.
Tunasema kwa kuwa CUF haikubaliani na maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, juu ya Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF…
Na kwa kuwa Profesa Lipumba anasema vikao vya CUF vya Agosti 21 na Agosti 28, mwaka huu vilivyomwondoa madarakani si halali…
Na kwa kuwa watu wengine wanaendelea kuamini kuwa Profesa Lipumba anatumiwa kuisambaratisha CUF…
Tunadhani ni muhimu watu wajiondoe kwanza kwenye daraja la uanachama wa vyama vyao na wahoji na kutafakari yafuatayo:
Ni kitu gani kinachomfanya Profesa Lipumba kung’angania kurejea kwenye uenyekiti wakati mazingira yaliyomfanya aache uenyekiti huo hayajabadilika (Lowassa bado yumo Upinzani)?
Na ni kwa nini askari polisi wamekuwa nyuma yake kuhakikisha kuwa anavuruga mikutano ya CUF?
Je, Profesa Lipumba ni mwema kiasi gani, kwamba hana historia ya kutumika huko nyuma katika masuala ya kukipa chama kingine manufaa ya kisiasa?
Ni nani miongoni mwa wana-CUF na Msajili wa vyama vya Siasa ametumia katiba ya CUF vizuri kujenga hoja katika mtafaruku huu?
Tunasema tutafakari kiyakinifu na kupata majibu ya maswali haya na kuja na suluhisho kabla ya kutoa lawama kwa kuongozwa na itikadi za vyama.