25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hatua za tahadhari zilizochukuliwa na Serikali

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

SERIKALI imezitaka mamlaka zote na wananchi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na jirani kuchukua hatua za tahadhari ikiwemo kuwahamisha wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi kupunguza madhara ya kimbunga Kenneth na mafuriko.

Akitoa kauli ya Serikali jana bungeni kuhusiana na hali hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alizitaka mamlaka zote na wananchi wa mikoa hiyo kuchukua hatua za tahadhari.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuwahamisha wananchi wanaoishi kando ya Bahari ya Hindi kuondoka katika maeneo ambayo yanatarajiwa kutokea kimbunga kabla hali ya hatarishi haijatokea.

Jenista alisema shughuli zinazofanywa kandokando na ndani ya Bahari ya Hindi, za uvuvi na usafirishaji wa anga na majini zinapaswa kusimama.

“Tunaendelea kusisitiza kamati za maafa katika ngazi zote maeneo husika kwa mujibu wa sheria tuliyonayo kufuatilia kwa karibu na kwa kina jambo hili.

“Naendelea kuelekeza uongozi wa ngazi zote kutoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutoa tahadhari katika mitaa mbalimbali na hatua mbalimbali za kuchukuliwa.

“Natoa rai kwa taasisi mbalimbali kuendelea kufuatilia na kujiandaa kutoa misaada ya kibinadamu endapo hali hiyo itajitokeza.

“Pamoja na kazi nzuri inayoendelea kufanyika kwa sasa, ninaendelea kuelekeza hatua stahiki zinachukuliwa ili kupunguza madhara ya kimbunga na mafuriko kama yatatokea kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa,” alisema.

Alisema Serikali kwa kuzingatia sheria ya maafa namba 7 ya mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa ya mwaka 2017, inaendelea kusisitiza kamati za maafa kupitia ngazi ya vijiji hadi wilaya kuhakikisha wanashirikiana na kushirikiana na wananchi.

“Vilevile wananchi wote wanaelekezwa kuchukua tahadhari na hatua katika suala zima la kushughulikia kujikinga kisheria kwa mujibu wa maelekezo ambayo tayari yametolewa.

 “Idara ya Maafa inaendelea kutoa taarifa na sisi sote tunafanya maandalizi yanayohitajika, tunaomba kufuatilia taarifa hizi za utabiri mara kwa mara zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa,” alisema Jenista.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles