23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Madhara kimbunga Kenneth kutikisa

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAKATI wananchi wa Mkoa wa Mtwara wakiendelea kuhama makazi yao kwenda maeneo salama kujikinga na madhara ya kimbunga Kenneth, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema madhara zaidi yataonekana leo katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Jana Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi, alisema wanatarajia kimbuka hicho ambacho kikiwa baharini spidi yake ni hadi kilomita 140 kwa saa, kitakapotua nchi kavu spidi ya upepo itapungua kufikia kilomita 100 kwa saa.

Alisema kutoka eneo ambalo kimbunga hicho kitatua nchini Msumbiji, madhara yake yatasambaa kilomita 600 hivyo yatagusa pia Mtwara, Lindi na Ruvuma.

“Ni matarajio yetu kuwa kimbunga hiki kitaendelea kusogea kuelekea maeneo ya pwani na mpaka kufikia kesho Aprili 26 (leo) nyakati za alfajiri, kimbunga hiki kitakuwa kinatua nchi kavu na kitakuwa katika ardhi ya Msumbiji na kinatarajiwa kutua katika maeneo ya latitude 12.3 kusini na longitude 39.4 mashariki.

“Na kitakuwa umbali wa kilometa 237 kutoka pwani ya Mtwara na kwa kawaida kimbunga kinapotua, kinapunguza ile nguvu ya ule upepo, tunatarajia kuwa upepo utapungua kutoka zile kilometa 140 kwa saa, zitafikia kilometa 100 kwa saa wakati kitakapokuwa kimetua.

“Lakini upepo huu wa kilometa 100 kwa saa katika nchi kavu ni upepo mkubwa, ni upepo ambao unaweza ukasababisha athari katika maeneo husika. Tumejaribu kukiangalia kimbunga hicho katika mzunguko wake ambao unaweza kuleta athari ni mzunguko wa aina gani, tumeona kwamba ni kama kilometa 600.

“Kwahiyo utaona kwamba kutoka katika eneo lile la Msumbiji ambalo kimbunga kitakuwapo, ukichukua kilometa 600 ina maana ni kuingia ndani katika maeneo ya nchi yetu inaweza kufika maeneo ya Lindi, maeneo ya Ruvuma na eneo lenyewe la Mtwara likiwa ndani. Kwahiyo ni vema tuchukue tahadhari,” alisema Dk. Kijazi.

Alisema athari zinazoweza kutokea kutokana na kimbunga hicho ni pamoja na mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, kuharibiwa mazao mashambani, uharibifu wa miundimbinu na kuongezeka kwa kina cha maji baharini kutokana na upepo kuvuta maji ya bahari na kuyasogeza nchi kavu.

Dk. Kijazi alisema kimbunga hicho kitaathiri shughuli za usafiri ikiwamo usafiri wa anga, majini na nchi kavu, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanakuwa katika maeneo salama na kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Alisema kimbunga cha ukubwa huo ni kama cha kwanza kufika katika maeneo ya Tanzania, japo mwaka 1952 Tanzania ilikumbwa na kimbunga kilichofika maeneo ya Mkoa wa Lindi ambayo hata hivyo hayakuwa na watu wengi kwa wakati huo na hakukuwa na miundombinu mingi ambayo ingeweza kuharibiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles