Na PENDO FUNDISHA-MBEYA
HATIMAYE Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wameachiwa kwa dhamana baada ya kukaa mahabusu kwa muda wa siku 24.
Washtakiwa hao wawili walikamatwa Januari 16 mwaka huu na walifikishwa mahakamani kwa madai ya kutoa maneno ya fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Sugu na mwenzake walipewa dhamana ambayo masharti yake ni bondi ya shilingi milioni tano kila mmoja na kwamba wajidhamini wenyewe baada ya kufanyika makubaliano ya upande wa Jamuhuri na ule wa utetezi.
Uamuzi wa kuwapa dhamana ulifikiwa jana saa moja usiku licha ya kufikishwa mahakamani hapo na shauri lao kuanza kusikilizwa kuanzia saa tatu asubuhi.
Sugu na mwenzake walitimiza masharti ya dhamana na baada ya kuachiwa, hakimu alisema kesi hiyo inatarajiwa kutolewa hukumu Februari 19, mwaka huu.
Awali kabla ya kupata dhamana, shahidi upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Modestius Chambu, alikiri mbele ya mahakama kwamba maneno ya fedheha yanayodaiwa kutolewa na Mbunge Mbilinyi (Sugu) dhidi ya Rais Magufuli kuwa si mazuri na yalisababisha hali ya uvunjifu wa amani.
Shahidi huyo ambaye ni wa tano kati ya mashahidi saba wa upande wa mashtaka, aliyasema hayo jana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Mbeya, mbele ya Hakimu Michael Mteite.
Akimwongoza shahidi huyo, Wakili upande wa utetezi, Peter Kibatala, akisaidiana na Faraji Mangula, aliiambia mahakama hiyo kwamba wapo tayari kuendelea na shauri hilo huku akiomba kinga kwa mahakama hiyo kuhakikisha mashahidi wengine muhimu akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makalla, aliyeandikiwa hati ya kuitwa mahakamani hapo anatokea bila ya sababu.
Akijibu maswali kadhaa aliyoulizwa na Wakili wa Serikali, Joseph Pande, likiwemo swali la ufahamu wake kuhusu maneno ya fedheha dhidi ya rais, shahidi huyo alisema, maneno hayo si mazuri na kwamba yaliweza kuleta hali ya uvunjifu wa amani.
Akijibu kuhusu taratibu za ukamataji washtakiwa zilivyotumika, Chambu, aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wote walikamatwa kwa taratibu za kipolisi na kwamba zilizingatia sheria za makosa ya jinai, huku akisisitiza kwamba hatua ya yeye kumpigia simu Mbunge ni kutokana na hadhi aliyonayo ya ubunge.
Shahidi namba nne katika upande wa utetezi, Grace Malya, ambaye ni mke wa mshtakiwa namba mbili, Masonga, aliithibitishia mahakama hiyo kwamba mshtakiwa huyo ambaye ni mume wake hakuhudhuria mkutano huo kwani alikuwa nyumbani akimpa matibabu ya mgongo.
“Desemba 30, 2017 ambayo ndiyo siku ya mkutano, majira ya saa mbili asubuhi mume wangu alikwenda kwenye majukumu yake lakini majira ya saa saba nilimpigia simu na kumtaarifu kwamba mgongo unanisumbua hivyo alirejea nyumbani na kuanza kunipa matibabu na baada ya hapo hakutoka,” alisema.
Shahidi wa tano ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Boid Mwabulanga, ambaye alikiri kuhudhuria mkutano huo lakini hakusikia lugha zozote za fedheha zilizotolewa na Mbunge huyo.
Mwabulanga, aliieleza mahakama hiyo kwamba, katika mkutano huo, Katibu wa Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, hakuhudhuria mkutano huo na wala hajawahi kumwona kwenye mikutano kadhaa ya chama iliyowahi kufanyika ukiwemo mkutano huo wa Mbunge Sugu na wala hafahamu sababu zilizosababisha ashindwe kuhudhuria mkutano huo.