31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WANASAYANSI WAZALISHA MAYAI YA BINADAMU

EDINBURGH, Uingereza

KWA mara ya kwanza katika historia, hatimaye  wanasayansi nchini Uingereza wamefanikiwa kutengeneza kwa maana ya kuzalisha na kukuza mayai ya binadamu kwenye maabara mafanikio ambayo yametajwa kuwa yataleta matumaini kwa wanawake wasio na uwezo wa kuzaa.

Kazi hiyo ambayo imewachukua miongo wanasayansi hao wa Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza, inaelezwa waliondoa seli za yai kutoka tishu za ovari (ovary tissue) katika hatua za mwanzo za ukuaji na kuzikuza hadi kufikia hali ya mayai hayo kuwa tayari kupandikizwa mbegu za kiume.

Mara baada ya kukuzwa katika maabara, mbinu hiyo itarahisishia wanawake ambao wanapandikizwa mbegu za kiume kwa njia ya  In Vitro Fertilization (IVF) kwa kuhitaji tishu ndogo badala ya hatua mbalimbali za upandikizwaji.

Kwa mujibu wa mtandao wa Telegraph, hii imeonyesha kuwepo kwa ufanisi na inaweza kuwasaidia wanawake ambao hawana uwezo kuzalisha mayai kiasilia au kushindwa njia ya IVF.

Wanasayansi hao wamesema pia njia hiyo inaweza kuhifadhi uzazi wa wagonjwa wa saratani, lakini pia italinda uzazi wa wanawake wanaoendelea na matibabu ya ugonjwa huo  ambao wengi wao sasa wanaachwa ikiwa hawawezi kutunza mayai yao.

Utafiti huo unaweza kuwa muhimu hasa kwa wasichana ambao hawajapitia kipindi cha kubalehe. Kwa sasa tishu zao za uzazi zinaweza kuchukuliwa kabla ya matibabu na kugandishwa kwa matumizi ya baadaye.

Kwa mujibu wa watafiti hao, mbinu ya kukuza mayai ya binadamu inaweza kuwa njia mpya za kuhifadhi uzazi.

Taarifa ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC), inasema itakuwa fursa ya kuchunguza jinsi mayai ya binadamu yanavyozalishwa katika mwili wa binadamu kitu ambacho bado ni kitendawili kwa wanasayansi.

Wataalamu hao walisema ni hatua ya kusisimua, lakini kazi zaidi ilihitajika kabla ya kutumika kwenye kliniki.

Watafiti hao wanaelezea kuwa wanawake huzaliwa na mayai yasiyokomaa katika ovari (ovaries) zao ambayo yanaweza yakakua au kukomaa kikamilifu baada tu ya kubalehe.

“Inahitaji uangalifu wa kudhibiti hali kwenye maabara pamoja na viwango vya hewa, homoni, na protini zinazochochea ukuaji na utunzaji wa mayai.”

Wakati wanasayansi hao wameonesha kuwa inawezekana, mbinu iliyochapishwa katika jarida la Uzazi wa Binadamu (Molecular Human Reproduction), linasema mbinu hiyo bado inahitaji uboreshaji.

Mara nyingi kumekuwepo na upungufu kwa sababu asilimia 10  ya mayai hufikia katika hatua ya kukomaa.

Mmoja wa Watafiti hao, Profesa Evelyn Telfer, aliiambia BBC kuwa: “Ni furaha sana kupata ushahidi wa kuonesha kuwa inawezekana kufikia hatua kwa binadamu.

“Lakini hilo linapaswa kuangaliwa kwa kazi nzima iliyohitajika ili kuboresha hali ya mayai na kupima ubora wa mayai.”
Watafiti hao wanasema mayai hayo huhitaji kupoteza nusu ya chembechembe za urithi (genetic material) wakati wa kukua, vinginevyo kutakuwa na vinasaba vingi (DNA) baada ya kupandikiza mbegu za kiume.

Wanaelezea kiwango hicho kinawekwa ndani ya (miniature cell) kinachoitwa polar body, lakini katika utafiti wa polar body imeonyesha kuwa ilikuwa kubwa sana.

“Hii inaleta wasiwasi, lakini ni moja ya njia tunayoweza kushughulikia na kuboresha teknolojia,” alisema Profesa Telfer.

Alisema utafiti uliofanywa katika mayai ya panya na kufanikiwa miaka 20 iliyopita, ilionyesha teknolojia  hiyo inaweza kutumika katika kuzalisha wanyama hai.
Mshauri wa uzazi wa wanawake katika hospitali ya Hammersmith, Stuart Lavery, alisema: “Kazi hii inawakilisha hatua halisi katika ufahamu wetu.”

Mkurugenzi wa utafiti wa mbegu za mimea katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Profesa Azim Surani, alisema: “Tabia ya molekuli na uchambuzi wa chromosom inahitajika kuonyesha jinsi hizi seli za yai zinalinganishwa na mayai ya kawaida.

“Inaweza kuwa na manufaa kupima uwezekano wa maendeleo wa mayai katika maabara kwa hatua ya blastocyst, kwa kujaribu mfumo wa upandikizaji wa mbegu za kiume (IVF),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles