HATIMA ya nyumba zilizojengwa maeneo ya mabondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salam itajulikana leo kama zitabomolewa au laa.
Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, inatarajia kutoa uamuzi huo, baada wananchi kufungua kesi wakipinga kubomolewa nyumba zao.
Uamuzi huo, unatarajiwa kutolewa mahakamani hapo mbele ya Jaji Panterine Kente wa mahakama hiyo baada ya wananchi wanane kwa niaba ya wenzao wanaoishi katika maeneo hayo kufungua kesi kupinga hatua ya ubomoaji.
Wadaiwa katika kesi hiyo, ni Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo ambapo ombi la msingi la wananchi hao, ni kuitaka mahakama iwape kibali cha kesi ya msingi ya uwakilishi wa kupinga ubomoaji wa nyumba hizo.
Hata hivyo kabla ya ombi hilo kutolewa uamuzi , mawakili wa wananchi hao akiwamo Abubakari Salim, waliwasilisha ombi la kuitaka mahakama itoe amri ya kuitaka wadaiwa katika shauri hilo kusitisha ubomoaji na hali ibaki kama ilivyo sasa.
Wakili huyo, alidai wanaomba hali hiyo ibaki hadi hapo watakapopewa kibali cha kufungua kesi ya msingi na kutolewa uamuzi.