27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli awapa majukumu CAG, DPP

Dk.-John-P-J-MagufuliNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli kwa nyakati tofauti jana, alikutana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga na kuwapa majukumu yatakayokwenda na kasi ya  Hapa Kazi Tu.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kaimu Mkurungenzi wa Mawasiliano Ikulu, Greson Msigwa, ilisema Rais Dk. Magufuli amemwagiza Profesa Assad  kuona njia sahihi ambayo itasaidia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

“Hadi mwaka juzi, Tanzania ilikua inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya pato la Taifa, ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikua inakusanya asilimia 19…hakuna sababu za msingi za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo,” ilisema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikutana na DPP Mganga na kufanya naye mazungumzo ya kina yaliyojikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi yake inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu yake.

Taarifa hiyo imesema viongozi hao wamezungumzia umuhimu wa kuwahimiza Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza wajibu wake bila kumwonea mtu.

Mufti

Pia Rais Dk. Magufuli, alikutana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Ally ambaye alimpongeza Rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake.

Mufti Abubakar, alisema Waislamu wote wanamuunga mkono na kumwombea kwa mwenyezi Mungu ili aendelee na juhudi hizo.

“Kwa niaba ya Waislamu tunataka kumweleza kazi anayoifanya tunairidhia na tunamwomba aendelee kuifanya wala asiogope na kauli yake ya Hapa Kazi Tu iendelee, kwa sababu inaonesha  sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri,” alisema Mufti.

Bulembo

Kiongozi mwingine aliyekutana na Rais Magufuli, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo ambaye alimpongeza Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020.

Taarifa hiyo, imesema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk. Magufuli.

“Tunafurahi  yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa ada za shule za msingi na sekondari,”ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles