KWENYE maisha ni kosa kubwa kujiaminisha au kumkubali mtu fulani kuwa mtu huyu ni wa aina fulani pasipo kukaa naye kwa muda mwingi, muda ambao utakufanya uigundue tabia ya ndani kabisa ya mwanadamu huyo na hivi ndivyo ninavyoweza kuizungumzia Serikali ya Awamu ya Tano iliyo chini ya Rais Magufuli.
Serikali hii ukiamua kuipatia sifa kwenye kipindi hiki cha mwanzo basi bila shaka unaweza kusema hii ni Serikali ya kazi tu na ndivyo wananchi wengi wamekuwa wakiipatia sifa kuwa ni Serikali inayorejesha matumaini kwa wananchi, lakini kabla hata muda haujapita nimefanikiwa kuiona sifa ya Serikali hii, Serikali ambayo imeonekana na kila aina ya ujasiri kwenye kushughulikia watu kadhaa ambao walionekana kuwa hawako kwenye mstari ulionyooka, lakini baada ya kupita muda kidogo nimeanza kuiona sura ya Serikali hii ambayo ilikuwa imefichwa na matukio mengine kama utumbuaji wa majipu lakini baada ya kuiangalia kwa jicho la pili nikabaini ukiacha ile kauli mbiu yao ya ‘Hapa Kazi tu’ inawezekana ikawa imehamia kwenye ‘Hapa hofu tu’ Kwa nini hapa hofu tu?
Kwenye maisha ukiweza kumuua Simba basi bila shaka watu wengi watakutambua kama shujaa na jasiri maana ni mara chache kusikia mwanadamu kamuua Simba ila kusikia kuwa Simba kaua mwanadamu sio ajabu japo ni tukio la kuhuzunisha, ila kwa uhakika kabisa ni kuwa ukiua Simba kisha ukaja kufa kisa ulikuwa unamkimbia panya au mende sifa ya ushujaa na ujasiri wako wote itatoweka maana maswali yatakayokuwapo ni kuwa iliwezekanaje ukapata ujasiri wa kuua Simba lakini ukakosa ujasiri mbele ya panya au mende? Na kwangu mimi inawezekana kabisa wewe ni mwoga lakini sifa yako ya uoga ilifichwa na tukio lako la kuua Simba lakini kwa sababu kwenye ukweli uongo hujitenga ikaja kubainika kuwa wewe ni mtu wa hofu japokuwa hapo awali hukutuaminisha hivyo na hivi ndivyo ninavyoweza kuielezea Serikali ya Awamu ya Tano.
Inawezekana vipi ukatumbua majipu ya bandari, majipu ya watumishi hewa, majipu ya TRA, majipu ya TAKUKURU, majipu ya sukari ila ukaja kuzuia kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja? Wananchi mmetupiga danadana wee mwishowe mmefikia kwenye mlichokihitaji maana mwanzo mlisema kuwa TBC haitarusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kwa kuwa Serikali haina pesa hivyo Bunge litaruka likiwa limerekodiwa huku mkifahamu wazi matokeo ya kurusha kitu kilichorekodiwa, wananchi wakalalamika wee mkaweka masikio pamba mkasonga mbele kwa mbele kama wimbo wa chama fulani.
Mwanzo haikuonekana kama shida kubwa kwa sababu vituo vingine vilikuwa na nafasi ya kurusha wananchi wakasema sawa, ila mmeenda mmerudi nafikiri mkafanya maazimio yenu ya hofu mkitambua kabisa kuwa mnakuja kwenye Bunge la Bajeti hivyo macho na masikio yetu yalitakiwa Dodoma mkaamua kuzuia kabisa vyombo kuingia bungeni na kurusha matangazo kwa kisingizio cha kuwa mpaka studio za Bunge zitengenezwe huu ni woga na hii si sawa.
Sisi wananchi ndio tunaolipa kodi hivyo tunataka tuone kodi yetu inatumika vipi, sisi wananchi ndio mabosi wa wabunge na sisi ndio tuliowatuma hivyo tunataka kuona wanafanyaje kazi huko tulipowatuma kama wanalala tuwakatae kama walivyokataliwa wengine kwenye uchaguzi uliopita, hainiingii akilini tunapokataa Bunge lisirushwe moja kwa moja halafu bado tunaendelea kukimbiza Mwenge huu ni woga uliokithiri, Rais anafanya ziara za kushtukiza kutafuta majipu, wizara na mawaziri wake na vivyo hivyo na mpaka kwa watumishi wa umma wengine nao wanatafuta majipu wayatumbue lakini cha kustaajabisha ni kuwa inapofika muda wa kuwaonesha majipu yalipo wao hawataki wananchi tuyajue huu ni woga.
Richmond tuliijua kwa sababu ya kulifuatilia Bunge na mijadala yake, Escrow tuliifahamu kwa sababu tulifuatilia mijadala yake ya Bunge iliyorushwa moja kwa moja, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao tunayoipigia kelele nayo tuliizungumza juu yake kwa sababu tulikuwa tukifuatilia Bunge na hata jipu lilitumbuliwa kwenye uzinduzi wa Daraja la Kigamboni nalo lilishatajwa bungeni japo hamkulitumbua kwa wakati, mijadala hii na mengineyo mara nyingi tunaifahamu tunapofuatilia Bunge sasa unapotunyima haki yetu ya kutazama Bunge unataka hii mijadala tuifahamie wapi?
Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri sasa mnataka tufahamu vipi kama Serikali inashauriwa na kusimamiwa? Tuache siasa za hofu, kama ndio mbinu mliyofikiri mnaweza mkatumia ili kuwabana wapinzani basi ama kwa hakika mnakosea maana hapo tayari mmewapatia hoja, kwa bahati mbaya sijasikia mbunge yeyote wa chama tawala akilalama juu ya hili hivyo nafikiri haya ni maazimio ya chama kizima.
Kama mliyafahamu haya ni kwa nini mliamsha wananchi asubuhi wakajiandikishe na siku ya kupiga kura wawahi foleni halafu baada ya wao kuchagua viongozi hamtaki kuwaonesha ni kwa jinsi gani watu hao wanafanya kazi wakiwa ndani ya Bunge?
Hii si sawa kwa demorasia ya Taifa maana Rais ameendelea kupewa nafasi kwenye vyombo vya habari haswa haya masuala ya utumbuaji wa majipu huku wabunge wakiminywa nafasi yao hali itakayosababisha wabunge haswa wa upinzani kukosa nafasi huku wale wa chama tawala wakiendelea na safari kupitia mgongo wa Mheshimiwa Rais.
Taifa lenye demokrasia isiyo na mashaka huwa lina uwajibikaji na uwazi ila nashangaa ninapoona tunayawajibisha majipu hadharani ila tukitaka kuoneshwa majipu hamtaki. Kuna watu wanasema kuwa Bunge lilikuwa linafanya watu wasifanye kazi hii ni hoja isiyo na mashiko, hakuna mtu anayeacha kazi zake kisa anatazama Bunge na niwaulize tu hivi Mheshimiwa Rais alivyopiga simu kwenye kipindi cha luninga akidai kuwa anakifuatilia sana huwa hana kazi? Ufanyaji wa kazi ni mpangilio wa ratiba hivyo hoja hii haina mashiko.
Tafuteni majipu wee, tumbueni majipu wee ila kaeni mkitambua kuwa hata ukiua Simba watano lakini ukaja kufa na sababu ya kifo chako ikatokana na kumkimbia panya hakika itabaki historia kuwa uliwahi kuua Simba lakini ulikufa kwa woga.
Kama mliamua kukimbiza Mwenge hata kama hatuutaki basi tunaomba mtuoneshe Bunge hata kama hamtaki muachane na ‘HAPA HOFU TU’.