29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kuteketeza nyara pekee hakutapunguza ujangili  

meno ya temboKENYA imeweka historia mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuteketeza zaidi ya tani 100 za meno ya tembo pamoja na zaidi ya tani moja ya pembe za faru ambazo zilikamatwa kutoka kwa watu wanaotuhumiwa kuwa majangili. Hii si mara ya kwanza kwa Kenya kufanya kitendo kama hiki. Imekuwa ikichoma moto shehena za pembe za tembo mara kwa mara.

Hatua ya Kenya kuchoma hadharani meno ya tembo ambayo yamekamatwa kutoka kwa majangili ilianza Julai 1989 wakati Rais wa Kenya wakati huo, Daniel arap Moi alipowasha mwenge na kuteketeza rundo la tani 12 za meno ya tembo. Katika tukio jingine la karibuni linalofanana na hilo, Machi mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta alifanya tukio kama alilolifanya Jumamosi iliyopita pale alipochoma tani 12 za meno ya tembo yaliyonaswa kutoka kwa majangili.

Kwa matukio haya, Kenya ilijiwekea mfano wa kuigwa duniani kwani mataifa mengine mengi tu yamefuata mfano huo na yenyewe yakateketeza meno ya tembo yaliyokamatwa kutoka kwa majangili ambayo yalikuwa kwenye hifadhi zao.

Lakini wakati nchi nyingine zikiiga mfano huo wa Kenya, kumekuwa na kazi ngumu sana kuishawishi Tanzania kuchoma hifadhi yake ya meno ya tembo ambayo inaaminika kuwa ni kubwa kuliko zote duniani hivi sasa. Ingawa hakuna takwimu za uhakika zilizowahi kutolewa, inaaminika kuwa Tanzania inahifadhi zaidi ya tani 90 za meno ya tembo katika maghala yake. Sehemu kubwa ya meno haya yalikamatwa kutoka kwa majangili wakati mengine ni ya tembo waliouawa kihalali au kufariki wenyewe kutokana na sababu mbalimbali kama vile maradhi au uzee.

Hatua hii ya Kenya kuchoma meno ya tembo mara kwa mara imewezesha kubadilishwa kwa sera kadhaa, zikiwamo zile za kidunia, kuhusiana na masuala ya kudhibiti ujangili. Mabadiliko hayo yalifanyika pia baada ya kubainika kuwa ujangili umekuwa si tu ukiangamiza uchumi wa nchi kadhaa, bali pia umegeuka kuwa hatari kwa mazingira na maisha ya watu na viumbe wengine.

Ndio maana Shirika la Kimataifa la kupiga vita biashara ya viumbe walio hatarini kutoweka lijulikanalo kama CITES, limekuwa kila mara likipongeza hatua hii ya Kenya kwani inaaminika kuwa inasaidia kupunguza vitendo vya ujangili duniani. Kupitia mfano wa Kenya, CITES imewahi kuzishawishi nchi nyingi duniani kukubali pendekezo la kupiga vita biashara ya meno ya tembo duniani. Hivi sasa biashara hiyo hairuhusiwi mahali popote duniani.

Lakini sera hiyo, kwa upande mwingine, imekuwa ni kichocheo cha kukua kwa ujangili. Hii ni kwa sababu biashara ya meno ya tembo hivi sasa inafanyika kwa magendo. Na inafahamika kuwa biashara yoyote inayofanyika kwa kificho, basi bidhaa zake huuzwa kwa bei ya juu. Hilo ndilo linalowavutia majangili zaidi kwa sababu shughuli hiyo sasa inaleta kipato kikubwa.

Na kwa uthibitisho kuwa kuchoma meno ya tembo peke yake hakujaweza kusaidia kupunguza tatizo la ujangili, taarifa na tafiti zinaonyesha kuwa licha ya biashara ya meno ya tembo kupigwa marufuku duniani, lakini bado vitendo vya ujangili vilishamiri. Ilifika mahali ujangili ukasababisha kupungua kwa kiasi cha kutisha kwa idadi ya tembo hasa katika Bara la Afrika.

Hali hiyo imefanya kuwapo kwa shinikizo la kuitaka Tanzania nayo kuteketeza shehena ya meno ya tembo ambayo yapo kwenye hifadhi yake. Wengi wanataka kuiiga Kenya na kuteketeza nyara hizo kama njia ya kupiga vita vitendo vya ujangili.

Lakini wakati Tanzania ikishinikizwa kuchoma hifadhi yake ya meno ya tembo, bado haijaelezwa kinagaubaga Kenya imenufaika vipi na hatua yake ya kuchoma meno ya tembo mara kwa mara. Tulichokishuhudia ni Kenya kuathirika na ujangili kama ambavyo nchi nyingine ambazo hazina tabia ya kuchoma moto meno ya tembo zimeathirika.

Kama ilivyo kwa Tanzania na nchi nyingine, idadi ya tembo nchini Kenya nayo imepungua sana kutokana na vitendo vya ujangili. Kama kweli uchomaji wa meno ya tembo pekee ungekuwa unasaidia kupunguza ujangili, basi hili lisingekuwa tatizo kubwa nchini Kenya hivi sasa.

Lakini kwa upande mwingine, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa baada ya kutokea kwa hali hiyo ya ujangili wa kutisha ambayo ilihatarisha maisha ya tembo na wanyama wengine, mazingira, utalii na uchumi wa nchi kwa ujumla, Tanzania ilichukua hatua kadhaa kukabiliana na ujangili. Operesheni kadhaa zilifanyika nchi nzima.

Kwa mujibu wa taarifa hizi karibuni, hatua hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujangili kiasi kuwa idadi ya tembo, ambayo ilishuka kwa kasi ya kutisha, imeanza kuongezeka. Utafiti mwingine uliofanywa mwaka jana mathalani ulionyesha kuwa tembo katika mfumo wa Hifadhi ya Taifa ya Selous ambao walikuwa wanatoweka polepole kutokana na vitendo vya ujangili wameanza kuongezeka kwa kasi baada ya Serikali kufanikiwa kudhibiti kwa ukamilifu vitendo hivyo vya ujangili.

Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Tembo iliyomalizika Mei, 2015, wanyama hao adimu ulimwenguni katika sekta ya utalii wameanza kuongezeka na kutoa matumani mapya ya kuwanusuru kutoweka.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii ilionyesha mathalani katika kipindi cha mwaka mmoja pekee cha kati ya 2014 hadi Mei, 2015, idadi ya tembo hao iliongezeka kutoka 13,000 hadi kufikia 15,000. Kabla ya kutolewa kwa matokeo ya sensa hiyo hiyo mpya, utafiti uliofanyika mwaka 2007, ulibaini kuwapo tembo zaidi ya 70,000 katika mfumo huo wa Selous.

Mafanikio hayo yalipatikana kutokana na hatua nyingine za kudhibiti ujangili ambazo hazihusishi kuchoma moto shehena ya meno ya tembo. Ni kweli kuwa uchomaji wa meno ya tembo unaweza kusaidia kuionyesha dunia kuwa biashara ya nyara inachukiza, lakini iwapo itachukuliwa kama hatua pekee, haiwezi kuleta matokeo mazuri.

Kwa upande mwingine hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika miaka ya hivi karibuni kukabiliana na ujangili zimeonyesha kuwa kuna uwezekano wa kupunguza au kutokomeza kabisa ujangili kwa kuongeza udhibiti. Hivyo, wakati watu na taasisi wanaishinikiza Serikali kukubali kuchoma moto shehena ya meno ya tembo iliyohifadhiwa, wafahamu pia kuwa hatua hiyo pekee haiwezi kusaidia kupunguza ujangili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles