LONDON, UINGEREZA
JARIDA la Sunday Times limeripoti kuwa baadhi ya vigogo wa chama tawala cha Conservative nchini hapa wanataka Waziri wa Fedha, Philip Hammond kuwa Waziri Mkuu badala ya Theresa May.
Mawaziri hao wanamwona Hammond kuwa mtu mwafaka wa kuliongoza taifa hilo katika mchakato mgumu wa Uingereza kujiondoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit.
May alishindwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge mapema mwezi huu, ambao aliuitisha kabla ya wakati akitarajia kumpa mamlaka zaidi katika mazungumzo ya Brexit.
Hata hivyo, Waziri anayehusika na Brexit, David Davis amesema alimshauri May kuitisha uchaguzi wa mapema na kushindwa kwao kupata wingi wa viti umebadilisha mambo katika mazungumzo kati ya Uingereza na EU.
Davis ameongeza kuwa anadhani wana waziri mkuu mzuri na hivyo hakuna haja ya kuwepo ushindani katika uongozi na kuwa ana imani watafikia makubaliano mazuri na EU.