MTAALAMU: MIWANI ZA ‘MTAANI’ NI HATARI KWA WATUMIAJI

0
2553

 

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA


BAADHI ya Watanzania wapo hatarini kupofuka kutokana na  vitendo vya kununua miwani mitaani na kuzivaa kama urembo bila kupimwa macho, jambo ambalo ni hatari kwa macho yao, imeelezwa.

Kutokana na hali hiyo Serikali imeombwa kupiga marufuku  uingizaji wa makontena ya miwani  nchini kiholela  sambamba na uuzwaji mitaani na badala yake ziuzwe katika vituo maalum vilivyo na vipimo na watalaam wa macho.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Daktari wa Macho kutoka Kituo cha Makongoro kilichopo jijini Mwanza, Ereneo Kalisa, wakati akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake juu ya sababu ya ongezeko la Watanzania kuvaa miwani.

Kalisa alisema  miwani ni dawa kama  zilivyo dawa zingine zinazotolewa na watalaamu wa afya baada ya mgonjwa kupimwa, hivyo hivyo miwani inapaswa kuvaliwa na mtu ambaye amepimwa macho, lakini  hivi sasa uvaaji wa miwani umegeuka kuwa urembo hasa kwa vijana kitendo ambacho ni hatari kinachoweza kusababisha upofu.

Alisema yapo mambo mengi yanayosababisha mtu na tatizo la macho kama  kuvaa miwani bila kupima, umri, kukaa sana katika kompyuta, kusoma  kwa muda mrefu, shinikizo la damu, kisukari, presha ya macho, unywaji wa vileo vikali, uvutaji wa sigara na ulaji wa vyakula fulani.

“Watanzania wataendelea kuharibikiwa macho kutokana  na uvaaji wa miwani wanayonunua mitaani, wanapaswa  kutambua miwani yoyote inayotengenezwa ina namba zake hata ile inayouzwa mitaani.

“Sasa wafanyabiashara wasio watalaamu wa macho  wanapokwenda huko  nje wananunua na kuweka kwenye makontena ovyo ovyo  ambapo zile namba zinazobandikwa hutoka.

“Sisi kama watalaamu tunapoagiza miwani huwa tunazingatia ubora na aina ya miwani, pia hatumuuzii mtu bila kumpima na kumpa ushauri, tunajua ipo ya mbonyeo inayoona mbali, mbinuko ambayo ni ya kusomea karibu, ipo ya jua ama mwanga, pia ipo miwani ya kubandika ambayo inatumiwa na wanamichezo na waogeleaji maarufu kwa jina la ‘contact lens’.

“Sasa unapovaa miwani bila kupimwa tatizo la macho yako, unaweza kusababisha upofu wa ghafla kwa kuwa mishipa ya macho itakuwa inafanya kazi ya ziada ya kupambana na lenzi ambayo si sahihi katika jicho.

“Kuna uwezekano wa mishipa ile kulegea, ni wakati mwafaka wa  Serikali kutangaza vita kwa miwani ya mitaani kama ilivyofanya katika dawa za kulevya, vipodozi feki na simu feki vinginevyo madhara yatakuwa makubwa,”alisema.

Akizungumzia sababu ya watoto wadogo kuvaa miwani, alisema  yapo matatizo ya macho ya kurithi ambayo huzaliwa nayo akiwa na uoni hafifu, hivyo huwa na miwani yake.

Pia alisema tatizo lingine ni mtoto kuanza kusoma akiwa mdogo na muda mwingi hulazimishwa kusoma kitendo kinachofanya mishipa ya macho kuchoka.

Alisema mara nyingi  tatizo hilo huwapata watoto wanaoishi mjini tofauti na wale wa vijijini ambao muda  mwingi huwa katika shughuli za kawaida.

Kuhusu  watu  wenye umri kati ya  miaka  12 hadi 28 nao hupata tatizo la macho ikiwa sabbu kubwa ni kukaa sana katika kompyuta ama kushinda akiwa anangalia katarasi muda mrefu.

Kalisa alisema watu wengi wanaofikisha umri wa miaka 40 na kuendelea mara nyingi hujikuta wakiwa na tatizo la macho na kushindwa kusoma maandishi madogo kwa karibu, hivyo inapaswa kupimwa na kupewa miwani sahihi na kuongeza kuwa yapo maradhi kadhaa ambayo mtu anapougua lazima macho yanakuwa na tatizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here