Na Safina Sarwatt, Mwanga
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kutenga eneo lenye ekari 54.66 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Hospitali hiyo itajengwa katika Mamlaka ya mji mdogo wa Mwanga katika Kitongoji cha Mikuyuni Ukanda Tambarare ya Magharibi hatua itakayowaondolea changamoto wakazi wa ukanda huo kusafiri kwenda Hospitali ya Wilaya ya Usangi iliyopo Ukanda wa Mlimani.
Akizungumza leo Jumamosi Februali 27, 2021 mara baada ya kutembelea eneo itakapojengwa Hospital hiyo Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Tadayo, amempongeza Rais Dk. Magufuli kwa kukubali kuwajengea Hosptali hiyo ambayo itawasaidia wakazi wa tambarare kupata huduma za matibabu karibu.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dk. Abdul Msuya, amesema kujengwa kwa hospitali hiyo ya wilaya katika eneo la Ukanda wa tambarare ya Magharibi utawasaidia wananchi wa ukanda huo kupata huduma hiyo karibu.
Awali, Mkuu wa Idara ya ardhi na maliasili wilaya ya Mwanga, Atufigwege Mwasumbi, amesema Halmashauri imefanikiwa kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 54.66 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa hospital ya Wilaya.
Amesema eneo hilo kimsingi ni mali halali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, eneo hilo lipo kitalu ‘D’ kwenye kiwanja namba 53, lenye ukubwa wa ekari 54.66 na kwamba eneo hilo lilitengwa tangu mwaka 1981.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Wilaya ya Mwanga, Jafari Kandege, amesema katika kutekeleza ilani ya Chama hicho ya 2021-25, Rais Dk. Magufuli ameweza kuisimamia vema ilani hiyo na kwamba eneo linalokusudiwa kujengwa hospitali hiyo ya wilaya itatosheleza mahitaji yote ya wakazi wa Ukanda wa Tambarare ambao kwa kipindi kirefu ndicho kilikuwa kilio chao.