Hadija Omary, Lindi
Halmashauri zote nchini zimeombwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuelekeza kwenye afya ya mama na mtoto kwa ajili ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Uzazi Salama kwa mama na mtoto Utepe Mweupe, Rose Mlay mjini hapa katika maadhimisho ya siku ya utepe mweupe.
Mlay amesema matokeo ya Halmashauri kutotenga bajeti ya kutosha katika huduma ya afya ya mama na watoto wachanga yanachangia kwa kiasi kikubwa kuajiri wahudumu wa afya wasio na taaluma afya kwa kuwa ni gharama nafuu kuwaajiri.
“Wajawazito 30 na watoto wachanga 180 wanapoteza maisha kila siku kwa matatizo ya uzazi ambayo yangeweza kutibika, pamoja na serikali kuongeza bajeti kwa huduma kamili na za msingi za uzazi wa dharura halmashauri hazitengi fungu mahususi na la kutosha katika mipango yao.
“Halmashauri 24 kati ya 180 pekee ambazo katika bajeti 2017/18 hawakuweka fungu hili mahsusi kwa ajili ya huduma za uzazi za dharura, lakini hata walioweka ilikuwa ni kiwango kidogo sana,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, Mkuu Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi amesema kwa kutambua umuhimu wa huduma za afya serikali imedhamiria kwa makusudi kukabiliana na changamoto hiyo kwa kupandisha bajeti ya afya kutoka bilioni 31 mwaka 2016/17 hadi kufikia bilioni 269 kwa bajeti ya 2017/2018 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.
“Hii ni dhamira tosha kwa serikali kukabiliana na tatizo la vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua kwa maana fedha hizi zinapotufikia zinakwenda kuimarisha na huduma ambazo zitazuia vifo hivyo,” alisema Zambi.