Na Ahmed Makongo
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bunda ilikadiria kutumia zaidi ya Sh bilioni 39.3. kutoka serikali kuu na kwenye vyanzo vyake vya ndani katika mwaka wa fedha 2016/17.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Amos Kusaja, alisema hadi Juni 30 mwaka huu, makisio yote yalikuwa ni kutumia zaidi ya Sh bilioni 41.5 na kuanzia Julai 2016 hadi Juni mwaka huu zimetumika zaidi ya Sh bilioni 28.9 sawa na asilimia 69.76 ya makisio ya matumizi yote.
Alikuwa akizungumza kwenye kikao cha mwaka cha baraza la madiwani mjini Bunda.
Alisema bakaa iliyokuwapo wakati wa kufunga mwaka wa fedha wa 2015/2016 ilikuwa Sh bilioni 2.1 na kufanya mapato yote kwa ajili ya matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo kuwa zaidi ya Sh bilioni 41.5.
“Bakaa iliyokuwapo wakati wa kufunga mwaka wa fedha wa 2015/2016 ni Sh 2,150,105,777 na kufanya mapato kwa ajili ya matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo kuwa Sh 41,532,391,729,” alisema.
Alisema mapato ya vyanzo vya ndani makisio yalikuwa ni zaidi ya Sh milioni 850.8 na hadi kufikia Julai mwaka huu, zilikuwa zimekusanywa zaidi ya Sh milioni 737.1.
Alisema kuwa ruzuku ya mishahara makisio yalikuwa ni zaidi ya Sh bilioni 30.7 na hadi kufikia Julai mwaka huu, walikuwa wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 21.5.
Kusaja alisema ruzuku ya matumizi mengineyo makisio yalikuwa ni zaidi ya Sh bilioni 1.3 na hadi kufikia Julai zilikuwa zimekusanywa zaidi ya Sh bilioni 1.2.
Kuhusu ruzuku ya miradi ya maendeleo alisema makisio yalikuwa ni zaidi ya Sh bilioni 6.4, ambapo kufikia Julai mwaka huu, zilikuwa zimekusanywa zaidi ya Sh bilioni 5.3.
Alisema makisio yote yalikuwa ni zaidi ya Sh bilioni 39.3 na hadi kufikia Julai mwaka huu zilikuwa zimekusanywa zaidi ya Sh bilioni 28.8 sawa na asilimia 37.33 ya makisio yote.
Hata hivyo, alisema kulikuwa na chanagamoto mbalimbali katika kukusanya mapato ya halmashauri kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani, mojawapo ikiwa ni upungufu wa vifaa vya elektroniki vya kukusanyia mapato hayo.
Changamoto nyingine ni kukosekana tafsiri ya matamko ya serikali yanayotolewa kuhusu ukusanywaji mapato kama vile ushuru wa mazao na ukosefu wa miundombinu kwenye minada.
Alisema halmshauri hiyo itabuni vyanzo vingine vya mapato jambo ambalo madiwani wote wakiongozwa na Mwenyekiti Isack Mahera walilikubali ili kusaidia kuongeza mapato kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.