24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

“Hakuna muda wa nyongeza miradi ya maji fedha za Uviko-19”-Mhandisi Mahundi

Na Derick Milton, Simiyu

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaagiza Mameneja wa Wilaya, Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) nchi nzima, kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi Uviko-19 inakamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Amesema kuwa hakutakuwa na nafasi ya maelezo kwa meneja yeyote ambaye atashindwa kukamilisha miradi hiyo kwa muda muafaka ambapo ameagiza miradi yote inatakiwa kukamilika Mei, mwaka huu.

Kikao kikiendelea..

Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo Machi 2, katika siku yake ya kwanza ya ziara yake mkoani Simiyu, ambapo akiwa wilayani Busega amemtaka meneja wa RUWASA wilayani humo ambao wanatekeleza miradi miwili ya Uviko -19 kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Amesema kuwa miradi yote ya Uviko-19 mbali na kukamilika ujenzi wake, inatakiwa kutoa maji na wananchi wanaanza kutumia na siyo kukamilika kwa kujengwa tu bali inatakiwa kabla ya muda huo ianze kutoa maji.

Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta fedha hizo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Uviko, ambapo moja ya njia za mapambano ni wananchi kunawa mikono kwa maji safi na tiririka.

“Kunawa maji safi ambayo ni tiririka ni lazima kila miradi ukamilike ujenzi wake kwa asilimia 100 na siyo kukamilika alafu tunaambiwa kuna kitu fulani hakijakamilika, hapana…tunataka maji yatoke na wananchi waanze kutumia,” amesema Mhandisi Mahundi.

“Kwenye hii miradi kama wizara hatuna Excuse (msamaha) kwa Meneje yeyote wa Wilaya, wala hatuna muda wa ziada kwa ambaye mradi utashindwa kukamilika kwa muda, tunataka miradi ikamilike kabla ya mwezi wa tano na itoe maji kwa wananchi,” ameongeza Naibu Waziri hiyo.

Aidha, amewataka mameneja kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi wanaojenga miradi hiyo kwani muda uliobaki ni mchache sana na inatakiwa kukamilika ndani ya muda muafaka.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya Wilaya Busega Meneja wa RUWASA wilayani humo Mhandisi Samson Gagala amesema kuwa walipokea zaidi ya Sh milioni 450 fedha za Uviko -19 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya maji.

Mhandisi Gagala amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika vijiji vya Badugu na Kalemela ambapo ujenzi wake kwa miradi yote miwili umefikia kiwango cha asilimia 25.

“Kukamilika kwa miradi hii yote miwili itahudumia zaidi ya wananchi 80,000, lakini katika Wilaya tunayo mingine ambayo inajengwa kwa fedha za lipa kulingana na matokeo (P4R) zaidi ya Sh milioni 900.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Gabriel Zacharia amesema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ni asilimia 65 kutoka asilimia 39 wakati RUWASA inaanzishwa.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kuwaleta fedha nyingi katika miradi ya maji, kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya Wilaya hiyo asilimia kubwa ya wananchi ndani ya Wilaya hiyo kupata maji safi na salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles