26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Ummy aagiza utafiti kubaini wenye matatizo ya usikivu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameagiza kufanyika utafiti wa kina kubaini watu wenye matatizo ya ukosefu wa usikivu nchini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa asilimia 5 ya watu duniani sawa na milioni 466 wana ukosefu wa usikivu na kati yao milioni 432 ni watu wazima na milioni 34 ni watoto.

Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wakipatiwa huduma ya uchunguzi wa afya ya masikio, pua na koo ambazo zimetolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana katika kuadhimisha Siku ya Usikivu Duniani.

Akizungumza leo Machi 3 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usikivu Duniani, amesema kwa sasa hakuna takwimu rasmi za tatizo hilo nchini na kwamba zilizopo ni za hospitali tofauti.

Kwa mujibu wa Ummy takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zinaonesha kati ya Julai 2020 hadi Juni 2021 wagonjwa 20,987 walihudumiwa katika idara ya masikio, pua na koo na kati yao 1,575 walibainika kuwa na ukosefu wa usikivu.

Aidha takwimu za Hospitali ya Rufaa KCMC zinaonesha kwa mwaka 2021 ilihudumia wagonjwa 300 wenye matatizo ya usikivu wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana ilihudumia wagonjwa 3,095
kati ya Januari 2020 hadi Januari 2022 katika kitengo cha masikio, pua na koo.

“Badala ya kusema asilimia tano tu ya watu ni lazima tupate takwimu sahihi za ukubwa wa tatizo hili, nakuagiza mganga mkuu wa serikali shirikianeni na wadau mbalimbali kufanya utafiti wa kina, tunaamini kabisa tunaweza kuzuia matatizo ya ukosefu wa usikivu,” amesema Ummy.

Amesema Serikali imeweka msukumo katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya masikio na kuwataka Watanzania kuchukua hatua kujikinga.

Waziri huyo amewaasa wananchi kuepuka kutumia dawa bila kuandikiwa na watoa huduma za afya kwani matumizi holela ya dawa yanachangia watu kupoteza uwezo wa kusikia au kuwa kiziwi.

“Epukeni kukaa mara kwa mara kwenye sehemu zenye kelele na matumizi ya spika za masikioni kwa muda mrefu kwa sababu yanachangia tatizo la ukosefu wa usikivu,” amesema.

Naye Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Fatma Kibao, amesema kliniki ya magonjwa hayo ilianzishwa mwaka 2020 ambapo ina madaktari bingwa wawili na kwa siku wanahudumia wagonjwa kati ya 15 hadi 21.

“Wagonjwa ni wengi na idadi kubwa ni wanawake na watoto, kuna uhaba wa majengo na vifaa, tukipata chumba cha kupimia usikivu tutapunguza rufaa kwa sababu inabidi wagonjwa waende Muhimbili,” amesema Dk. Fatma.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Bryson Kiwelu, amesema kati ya Januari 2020 hadi Januari 2022 wagonjwa 3,095 wamehudumiwa katika kitengo cha koo, pua na masikio na kati yao 1,671 waligundulika kuwa na matatizo ya masikio.

Aidha amesema wagonjwa 602 waligundulika kuwa na matatizo ya usikivu.

Katika kuadhimisha Siku ya Usikivu Duniani Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana inatoa bure huduma ya uchunguzi wa afya ya pua, koo na masikio.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Ili kuwa na usikivu bora maishani sikiliza kwa uangalifu’ ambayo inalenga kuhamasisha kila mmoja kulinda usikivu wake kwa kusikiliza kwa uangalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles