Paris, Ufaransa
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Antoine Griezman amekataa kufananishwa na wachezaji wakongwe wa timu hiyo, Zinedine Zidane na Michel Platini kwa madai safari yake bado ndefu.
Hatua hiyo imekuja baada mchezaji huyo kuonesha uwezo mkubwa katika mchezo dhidi ya Ujerumani ambao uliipa timu yake tiketi ya kucheza fainali ya Euro 2016 dhidi ya Ureno.
Katika mchezo huo, Griezmann alifanikiwa kufunga mabao mawili ya ushindi na kufanya hadi mwisho wa mchezo matokeo yawe 2-0 na kutinga fainali ya Euro 2016.
“Nina furaha kwa mafanikio yangu lakini bado nina safari ndefu katika maisha yangu ya soka hadi kuyafikia mafanilio ya Michel Platini ,” maneno ya Antoine Griezmann wakati akikataa kulinganishwa na nguli huyo wa soka nchini Ufaransa.
Kutokana na rekodi iliyonayo Ufaransa inaamini kwamba huenda wakatwaa kombe hilo katika mchezo utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Stade de France uliopo jiji la Paris.
Griezmann alisita kukubaliana na ukweli kwamba uwezo wake na juhudi binafsi zinamfanya kuwa miongoni mwa wakongwe mashuhuri wa taifa hilo.
Uwiano uliopo kati yake na wakongwe hao unatajwa kuwa chanzo pekee kinachomtambulisha mchezaji huyo bila kuzingatia timu anayocheza, aina ya mashindano au mwaka.
Katika Euro 1984, uhodari wa Platini wa kusakata soka ndio ulithibitika baada ya kumaliza akiwa na mabao tisa na kufanikiwa kuwa mfungaji wa michuano hiyo kwa kipindi hicho.
Nyota ya Zidane ilionekana katika Kombe la Dunia mwaka 1998, baada ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na kulisaidia taifa lake kunyakuwa kombe hilo.
Mchezo dhidi ya Ujerumani uliofanyika jiji la Marseille, Griezmann alionesha uwezo ambao haukuwahi kuonekana katika kipindi chake alichowahi kucheza soka la kuvutia.
Uwezo huo ndio unadaiwa kuifanya ngome ya Ujeruamni kuwa dhaifu na kuruhusu adhabu ya penalti ikiwa wiki chache tangu akose penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Hata hivyo nyota huyo ndio mwenye mabao mengi katika michuano hiyo baada ya kufikisha mabao sita na kuongeza uwezekano wa kuendelea kutajwa zaidi Ufaransa.
Inakumbukwa mchezaji huyo alitoa mchango muhimu kwa timu yake ya Atletico Madrid na kuiondoa Barcelona katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).