25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Rosa-ree Hip Hop yes, mapenzi no!

Rosa-ree
Rosa-ree

NA CHRISTOPHER MSEKENA,

UMEJENGEKA utamaduni ndani ya jamii yetu kuwa  muziki wa Hip Hop ni muziki wa kiume. Hali hiyo imetokana na ukweli kwamba idadi ya wasanii wa kiume ni kubwa kuliko ile ya wasanii wa kike kwenye muziki huo unaopendwa zaidi duniani.

Kama haitoshi imani hii ambayo haina mashiko mbele ya kizazi hiki kipya ilizifanya jamii nyingi za Kiafrika kuwatilia mashaka wachanaji wa kike waliojitoa ufahamu na kuzama kwenye muziki huo kuangalia watatazamwa vipi na ndugu, washkaji na mashosti zao na jamii yote inayowazunguka.

Wakati dunia ikiwaaangalia Mamc wa kike kama vile  Missy Elliot, Eve, Queen Ratifah, Lil Kim, Nicki Minaj na wengine kibao hapa Bongo, tunajivunia wachanaji wa mistari kama vile Rah P, Sister P, Zay B, Witnnes Kibonge Mwepec, Chemical, Cindy Rulz na Chiku Keto.

Nadhani pia itakuwa burudani kwako wewe msomaji na shabiki wa aina hii ya muziki pale ambapo nitakusogezea kichwa hiki kipya kutoka lebo ya The Industry inayomilikiwa na kundi la Navykenzo, anayeitwa Rosary Robert na jina la jukwaani Rosa-ree.

Swaggaz limepata taimu ya kupiga naye stori mbili tatu ili kufahamu mambo kadhaa kuhusu maisha na mtazamo wake juu ya muziki wa Hip Hop wenye ushindani mkubwa ndani na nje ya Bongo.

Swaggaz: Kwa mtu ambaye hakufahamu, Rosa-ree ni nani hasa?

Rosa-ree: Mimi ni Mchaga, mzaliwa wa Kilimanjaro na ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto watatu ambao wote ni wa kike kwa hiyo nina dada zangu wakubwa wawili ninaowafuata.

Swaggaz: Wasichana wengi wanapoanza kufanya muziki, familia zao zinakuwa na mashaka na wakati mwingine huwakataza kabisa wasijihusishe na muziki, wewe familia ilikuchukulia vipi?

Rosa-ree: Nakumbuka muziki nilianza kuupenda toka nikiwa mtoto na hata pale nilipoamua kutumia full taimu kwenye mishemishe za muziki familia yangu ilinipa sapoti, hakukuwa na tatizo.

Swaggaz: Tukirudi kwenye muziki, ulipata vipi dili la kusaini kwenye lebo kubwa kama The Industry?

Rosa-ree: Nilikutana na Nahreel mwaka jana mwishoni na nilikuwa nataka kufanya naye kazi zangu binafsi ila nilikuwa sifahamu kama ana wazo la kuanzisha lebo.

Baada ya muda kupita ndiyo akaniambia kuwa yeye na Aika wamenisikiliza kwa kina na wangependa kunisaini kwenye lebo yao. Kwa kweli nilikosa mpaka pumzi kwa furaha niliyokuwa nayo.

Swaggaz: Kuna changamoto zipi ambazo wasichana kama wewe hukutana nazo na kufanya wakate tamaa ya kuendelea na muziki?

Rosa-ree: Vikwazo kwa sisi wasichana hasa tunaofanya muziki wa Hiphop ni watu kutokuwa na imani kama wanadada wanauweza muziki huo wa rap kwa kudharau jinsia zetu.

Swaggaz: Wewe ni msichana mrembo mno, vipi upande wa mahusiano una mpenzi?

Rosa-ree: Kiukweli sipo tayari kuongelea mambo ya mapenzi. Kwa sasa kikubwa nafocus kwenye muziki kwanza.

Swaggaz: Wakati unaanza kutamani kufanya muziki wa Hip Hop, Mc gani alikuwa anakuvutia nje ya Bongo.

Rosa-ree: Navutiwa na marapa pamoja na wanamuziki wengi. Nampenda sana Kendrick Lamar, Wale, Lil Wayne na Sakodie wa Nigeria.

Swaggaz: Na hapa Bongo je?

Rosa-ree: Hapa nyumbani nawakubaki G Nako, Joh Makini na Young Dee kwa sababu wana vipaji vya kipekee mno.

Swaggaz: Kuna ishu ya wasanii kutumia dawa za kulevya, hili kwa upande wako unalitazama vipi?

Rosa-ree: Mimi naamini kwamba madawa ni lazima uyaendekeze ili yakuzoee, namaanisha kuyatumia au kutoyatumia ni maamuzi ya mtu. Ujana una tabu sana unajua, kwa hiyo utakuta wengi wanayatumia kwa kuwa wapo kwenye ujana.

Napenda kuwahimiza vijana wenzangu wasiangalie maisha ya leo tu wakumbuke na kesho pia. Kutumia dawa za kulevya kunafunga milango mingi ambayo ingeweza kuleta maisha mazuri hapo baadaye.

Swaggaz: Asante sana kwa muda wako.

Rosa-ree: Shukrani pia na wewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles