28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Jerry Muro apata balaa jingine

 Jerry Muro
Jerry Muro

NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kutangaza kumfungia mwaka mmoja Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, amekumbwa na balaa jingine baada ya kupata ajali ya gari.

Muro alikumbwa na mkasa huo jana akiwa anaendesha gari lake aina ya Harrier, saa mbili asubuhi wakati akitokea kijijini kwao Machame kuelekea Machame mjini kusalimia ndugu zake, ambapo gari hilo liliteleza na kugonga kwenye kisiki kilichokuwa pembezoni mwa barabara, jambo lililosababisha tairi la mbele kupasuka.

Akizungumzia ajali hiyo, Muro alisema imetokana na hali mbaya ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Kijiji cha Machame.

“Namshukuru sana Mungu nimenusurika, sijaumia ila gari ndio imeharibika sababu za mvua za rasharasha ambazo zimekuwa zikinyesha muda mrefu sasa, suala hili limekuwa likisababisha utelezi ukizingatia huku Machame kuna milima,” alisema Muro.

Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umesema hautambui maamuzi ya TFF ya kumsimamisha Muro mwaka mmoja pamoja na faini ya Sh 3,000,000, maamuzi yaliyofikiwa na kamati hiyo chini ya Mwenyekiti, Wilson Ogunde.

Katibu Mkuu wa Yanga, Deusdedit Baraka, alisema wao hawatambui maamuzi hayo kwa kuwa hawana taarifa yoyote.

“Sisi hatuna taarifa yoyote zaidi tumekuwa tu tukisikia kwenye vyombo vya habari, lakini taarifa rasmi kutoka TFF hatujaipata kwa hiyo hatutambui,” alisema.

Kwa upande wa TFF kupitia kwa Ofisa Habari wake, Alfred Lucas, alikiri  kutowasilishwa barua hiyo kwa Yanga.

“Ni kweli bado hatujawapelekea taarifa ya kimaandishi kwa kuwa hukumu ilitoka jioni, hivyo tunaiandaa ikiwa tayari tutawapatia,” alisema Lucas.

Mashtaka yaliyomtia hatiani Muro ni la kupingana na maelekezo ya TFF wakati wa maandalizi ya mchezo wa Yanga dhidi ya TP Mazembe wa Kombe la Shirikisho barani Afrika uliochezwa Juni 28, mwaka huu na kushindwa kulipa faini ya Sh 5,000,000 aliyopigwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF, Mei 5 mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles