Amina Omari, Handeni
Mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe, amewatoa hofu wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda vya kuchakata na kununua zao la muhogo wilayani humo kuwa ipo ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa.
Gondwe ameema hayo leo Jumatano Novemba 7, wakati akizungumza na wawekezaji waliofika wilayani humo kwa nia ya kutaka kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha kusindika bidhaa zitokanazo na zao hilo.
“Wananchi wamehamasika kwa wingi kulima zao hilo huku wakifuata ushauri na maelekezo wanayopewa na maofisa kilimo ili kupata muhogo wenye ubora.
“Nashukuru kuona Handeni ni eneo muhimu la kuja kuwekeza, pia msiwe na wasiwasi kuhusu ubora wa hii mihogo haina shida na mambo ya upatikanaji wa umeme, ardhi kwa ajili ya viwanda maeneo yapo na hayana migogoro.
“Handeni kuna mihogo bora na safi kuliko sehemu yoyote Tanzania kwa kuwa ina ardhi ambayo ina mbolea ya asili ambapo shina moja la muhogo inatoa hadi kilo 10 ukilinganisha na maeneo mengine Tanzania,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Mkufwe, amesema atahakikisha anatoa ushirikiano kwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika halmashauri hiyo ili kuwawezesha wakazi wa Handeni kupata soko la zao hilo kwani ni muda mrefu walikuwa wakitegemea zao moja la mahindi kama zao la biashara.