27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Giza nene kiwanda cha Mponde

mafuruNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

UAMUZI wa Serikali kutaifisha kiwanda cha chai kinachomilikiwa kwa pamoja na Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara (UTEGA)  na mwekezaji Kampuni ya Lushoto Tea Company Limited,  umetajwa kuwa haukuzingatia sheria na kanuni za uwekezaji.

Hatua hiyo ya Serikali ilichukuliwa Januari 29  mwaka huu na Msajiri wa Hazina, Lawrence Mafuru baada ya kikao cha uamuzi juu ya suala hilo.  Kiwanda hicho kilifungwa miaka minne iliyopita.

Kiwanda hicho kilifungwa kutokana na kinachodaiwa kuwa  mwekezaji   na Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara (UTEGA) kushindwa kuweka wazi mapato na matumizi ya kiwanda hicho kilichokuwa kikiendeshwa kwa ubia kati ya Lushoto Tea Company Limited na umoja huo.

Mmiliki wa Kampuni ya Lushoto Tea Company Limited iliyoingia ubia na UTEGA, Nawab Mulla, alisema uamuzi wa serikali kunyang’anya kiwanda hicho ulichukuliwa kinyume cha sheria kwa vile hivi sasa  nchi haina sheria inayoruhusu utaifishaji.

Mulla ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, alisema utaifishaji huo umeegemea katika maslahi ya  siasa huku akimtaja Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba kuwa ndiye alisababisha mgogoro hadi kiwanda kikafungwa.

Alisema hatua hiyo ya serikali ni kinyume na sheria zinazomlinda mwekezaji ambaye alipewa cheti na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kinampa uwezo wa kutafuta haki yake katika mahakama za kimataifa.

“Tumenyang’anywa kiwanda hata kabla ya miezi sita kupita kwa mujibu wa agizo la serikali kwa watu walionunua viwanda au mashamba na kushindwa kuyaendeleza …ni wazi kuna shinikizo la  siasa kutoka kwa mtu aliyeko juu serikalini.

“Mkataba wa mauziano unasema iwapo upande mmoja utashindwa kutekeleza masharti ya mkataba huo utatoa taarifa ndani ya siku 30 na upande wa pili utatoa majibu ndani ya siku 30.

“Kama pande zote hazikufikia mwafaka kitaitishwa kikao cha upatanishi baada ya siku 30 tangu pande mbili zilipojibizana ambazo ni siku 90, lakini utaratibu huo haukufuatwa na serikali,” alisema Mulla.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hatua ya serikali kunyang’anya kiwanda hicho kutaathiri wakulima wa chai ambao walikuwa wakitegemea zao hilo kuinua uchumi wao.

“Serikali ingeangalia chanzo cha mgogoro ni nini. Nakumbuka kiwanda hicho walimilikishwa wakulima na si mwekezaji ila  ulikuwapo   mgogoro lakini nashangaa kwa nini serikali imeamua kukichukua kiwanda na kumwondoa mwekezaji.

“Mwekezaji  hakumilikishwa na serikali bali wakulima ndiyo waliomtafuta wenyewe.

“Wakati ule tuliunda kamati ya mashirika ya umma na tulikwenda hadi Bumbuli na tuliandaa ripoti ambayo tuliiwasilisha Bungeni, tulipendekeza njia za kumaliza mgogoro huo, Serikali ilipaswa kurejea ushauri huo wa Bunge kumaliza mgogoro huo badala ya kukifunga   kiwanda,” alisema.

Ushauri wa POAC

Kamati ya POAC ilibaini makosa yaliyofanywa na serikali kushindwa kuingilia kati uvamizi wa watu katika Msitu wa Sakare uliopo Wilaya ya Korogwe ambao ulikuwa ukitumiwa na kiwanda hicho kupata  kuni za kuendeshea mitambo.

Wavamizi hao walifumbiwa macho na vyombo vya dola na msitu huo ukawa  unavunwa kuni na kuuzwa  katika viwanda vingine vya watu binafsi.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa mwekezaji   na washirika wake UTEGA, walikuwa hawajalipa deni lililobaki la Sh  milioni 370 kati ya Sh milioni 750 walizotakiwa kuilipa serikali kupitia Tume ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma (PSRC) pamoja na lililokuwa Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).

Fedha hizo zilikuwa  kama malipo ya ununuzi wa kiwanda hicho lakini wabia hao walikataa kumalizia deni hilo baada ya kunyang’anywa Msitu wa Sakare ambao kwa mujibu wa mkataba wa mauziano ulikuwa umejumuishwa.

Ripoti ya POAC ukurasa wa 34 na 35 ilishauri mwekezaji atendewe haki katika deni lake huku wakishauri Serikali ya Mkoa wa Tanga iondoe hali ya kutoaminiana baina yao na mwekezaji ili kudumisha amani.

Kikosi kazi cha Pinda

Baada ya juhudi mbalimbali kufanyika bila kufikia ukomo, Waziri Mkuu wakati huo, Mizengo Pinda aliitisha kikao mkoani Tanga na kutangaza kubaini makosa ya serikali yaliyosababisha kiwanda kufungwa ambako aliunda kikosi kazi (task force) ili kitoe mapendekezo kabla ya kufunguliwa kiwanda hicho.

Kikosi kazi hicho kilijumuisha maofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Hazina, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Viwanda na Biashara, CHC, Bodi ya Chai, UTEGA na Mwekezaji.

Kilitoa mapendekezo ambayo yaliridhiwa na waziri mkuu kwamba kiwanda kifunguliwe chini ya mwekezaji yule yule na serikali itapeleka msimamizi wa muda atakayekuwa akiangalia uendeshaji wa  kiwanda.

Waziri mkuu alisema serikali ingetoa gharama za awali za uendeshaji wa kiwanda hicho ikishirikiana na mwekezaji aliyekubali kutoa sehemu ya gharama ambazo zingetumika kufanya marekebisho kadhaa ya mitambo yake iliyoharibika kutokana na kukaa muda mrefu bila   kufanya kazi.

Kauli ya Mafuru
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema serikali iliamua kukichukua  kiwanda hicho kutokana na mgogoro uliopo baina ya wakulima na mwekezaji na sasa   inatafuta mwekezaji mwingine  kukifufua.

Kuhusu sheria ya utaifishaji   na muda wa kuvifungia viwanda visivyofanya kazi kwa mujibu wa mkataba, Mafuru alisema suala la Mponde ni tofauti na viwanda au mashamba yaliyoainishwa katika tamko la serikali.

“Hatujakichukua kiwanda kwa shinikizo la siasa, na kiwanda hicho ni tofauti na vile vilivyopewa miezi sita.  Lakini kuhusu mkopo wa benki kwa mwekezaji huyo awali ilipaswa kuuliza kwa sababu serikali haimtambui, lakini tutashirikiana nayo kwa kukifufua  kiwanda kifanye kazi na wao wachukue mkopo wao,” alisema Mafuru.

Januari azungumza

Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba ambaye anatuhumiwa kushinikiza Utega na mwekezaji kunyang’anywa kiwanda hicho ili apatiwe mfanyabiashara mmoja (jina tunalo), alimtaka mwandishi kufanya utafiti wa kina kuhusu suala hilo.

“Check your facts … when did I start working in this office?… This problem has been there for four years now and I only have one year in this office…., nikishiriki kushinikiza nikiwa kama nani wakati sikuwapo hata kwenye utumishi wa serikali… fanya utafiti vizuri juu ya habari unayoiandika ‘If you want to get serious readers’,” aliandika Makamba  katika ujumbe wake huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles