MKUU wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Paza Mwalima, amezuia kufanyika kwa maandamano ya wachimbaji wadogo wa madini wa Kijiji cha Dilifu ambao walitaka kuvamia eneo la Kampuni ya Jani Investment, inayomilikiwa na mwanasiasa, Crisanti Mzindakaya.
Wachimbaji hao wadogo wa madini ya dhahabu walikuwa wamepanga kufanya maandamano hayo jana kuanzia eneo la Dilifu hadi kwa Mkuu wa Wilaya yakiwa na lengo la kupinga uamuzi wa Wizara ya Nishati na Madini Kanda ya Magharibi wa kuwataka wachimbaji hao kusitisha shughuli zao.
Kutokana na hali hiyo wachimbaji hao walitakiwa kuondoka katika eneo hilo na kumpisha mwekezaji wa kampuni hiyo.
DC Mwalima, alilazimika kwenda katika eneo hilo na kusikiliza kilio cha wachimbaji hao wapatao 2,300, huku akiahidi kulipatia ufumbuzi suala hilo.