25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Siri majangili kutoroka yaanikwa

Tundu la mahabus*Polisi walichapa usingizi, waziri aagiza uchunguzi

Na Samwel Mwanga, Simiyu

NI umafia wa aina yake uliofanikisha watuhumiwa watatu, wakiwamo wa ujangili na mauaji kutoroka kwa kutoboa tundu kwenye ukuta wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Watuhumiwa hao, wawili wa ujangili na mmoja wa mauaji, walitoroka muda mchache baada ya kutoka mahakamani ambako walipelekwa kutokana na kesi zilizokuwa zinawakabili.

Tukio hilo la aina yake lilitokea Februari 19, mwaka huu saa nane usiku, ambapo inaelezwa kuwa watuhumiwa hao walitoroka wakati mvua ikinyesha baada ya kutoboa ukuta na kitu chenye ncha kali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bariadi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Audax Majaliwa, alisema kutokana na tukio hilo askari saba wanashikiliwa.

Alisema watuhumiwa hao kabla ya kutenda tukio hilo, Februari Mosi mwaka huu, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazowakabili.

Kaimu Kamanda Majaliwa alisema baada ya kusikilizwa kwa kesi zao, walirudishwa mahabusu katika kituo hicho cha polisi, wakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuhamishiwa katika gereza la wilaya.

Aliwataja watuhumiwa hao waliotoroka kuwa ni pamoja na Chiluli Sitta (28) mkazi wa kijiji cha Mwasangula Kata ya Itinje wilayani humo, ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi a mauaji.

Wengine ni Msanja Ndangule (45) na mtoto wake Paschal Masanja, wote wakazi wa Kijiji cha Sapa, Kata ya Itinje wilayani humo ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ujangili.

“ Watuhumiwa hawa walitumia sehemu ya bafu na choo ambayo kwa kawaida inakuwa imeharibika au kuloana sana kutokana na mkojo ambao ukojelewa na mahabusu.

“Kwa kawaida mkojo na simenti havipatani, tuna hofu kuwa sehemu hiyo ilikuwa haina ugumu hata kidogo,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.

Alisema kuwa pamoja na ukuta huo kuonekana umeharibiwa na mkojo hivyo kuwarahisishia watuhumiwa hao kutoboa na kutoroka, kulikuwa na uzembe uliofanywa na askari waliokuwa zamu pamoja na mkuu wa kituo hicho.

Kaimu Kamanda Majaliwa alisema katika mahabusu hiyo walikuwamo watuhumiwa sita, ambapo watatu walitoroka na wengine wawili walibaki, ambao ndiyo walitoa taarifa kwa askari kuwa wenzao wametoroka kwa kutoboa ukuta.

“Jambo la kushangaza kwanini wengine walibaki? Na hawa waliotoroka wanatoka kata moja, tuna hofu hapa kuwa kulikuwepo na njama, lakini kwa waliobaki walieleza kuwa waliona dalili mapema kwa wenzao kuwa wako kwenye mipango mikubwa,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.

Majaliwa alisema kuwa kutokana na tukio hilo tayari jeshi hilo limeanza kuchukua hatua za haraka, ambapo mpaka sasa askari saba wanashikiliwa ili kusaidia uchunguzi.

Aliwataja askari hao kuwa ni G. 8371 PC Adam, F. 9840 DC Hussen, D. 5582 Koplo Peter ambaye alikuwa kiongozi wa zamu siku ya tukio, G. 4806 PC John, G.8602 PC Yassin, H. 8410 PC Hery na WP. 1125 Hadija.

Kaimu Kamanda Majaliwa alisema kuwa baada ya hatua hizo kwa askari hao, taratibu nyingine za kushtakiwa kijeshi zitaendelea mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Alisema kuwa askari hao wanahusika moja kwa moja kwani licha ya mvua kunyesha, walitakiwa kufanya kazi ya kulinda kituo hicho pamoja na watuhumiwa hao, na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha walikuwa wamelala.

Kaimu Kamanda Majaliwa alisema hadi sasa watuhumiwa hao hawajapatikana na msako mkali unaendelea wa kuwatafuta ili kurudishwa gerezani kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashtaka yanayowakabili.

WAZIRI KITWANGA

Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, amesema ametuma timu ya uchunguzi wilayani Meatu ili kubaini chanzo cha watuhumiwa hao kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.

“Nawaomba muwe na subira, nimetuma timu ya wataalamu wangu kwenda kuchunguza kwa kina sababu za watuhumiwa hawa kutoroka wakiwa chini ya ulinzi…nitaujulisha umma baada ya kupokea ripoti.

“Naamini ripoti itakayokuja ndiyo itanipa picha halisi ya tukio hili, maana najiuliza ilikuwaje watu watoroke wakati wanakabiliwa na makosa mazito hivi,” alisema Waziri Kitwanga.

Alisema kutokana na hali hiyo, ametuma kikosi maalumu cha makachero kwa ajili ya kuwasaka kwa udi na uvumba watuhumiwa wote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles