26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

GGML waahidi kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inatarajia kukusanya fedha kiasi cha Dola za Kimarekani milioni moja (Sh bilioni 2.3) kupitia Kampeni ya GGM Kili Challenge 2022 inayotarajiwa kuanza Julai 15 hadi 21 mwaka huu.

Pia GGML imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia TACAIDS pamoja na wadau wengine kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi(VVU) na Ukimwi ili kufikia malengo ya sifuri tatu.

Mkurugenzi wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma (hawapo pichani) kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya GGM Kili Chalenge 2022 inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi. Kulia ni Meneja Mwandamizi wa masuala ya ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma.

Malengo ya sifuri tatu yanamaanisha kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Kauli hiyo imetolewa Alhamisi Juni 29, 2022 jijini Dodoma na Meneja Mwandamizi wa masuala ya Ubia kutoka GGML, Manace Ndoroma wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu uzinduzi kampeni ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2022.

Kampeni hiyo iliyoasisiwa na GGML mwaka 2002 inalenga kutunisha mfuko wa mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi kwa kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.

Pia kampeni hiyo inayosimamiwa na GGML na TACAIDS inalenga kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini na kushirikisha wadau kuchangia mwitikio wa  taifa dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI.

Alisema kampeni hiyo ambayo pia inashirikisha wadau kutoka nje ya nchi,  “Washiriki watapanda mlima Kilimanjaro kuanzia geti la Machame kwa njia ya miguu na wengine kwa baiskeli kisha kushukia geti la Mweka mkoa Kilimanjaro. Tunawakaribisha sana wadau wetu na makampuni mbalimbali kuchangia na kushiriki kampeni hii.”

Aidha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wake na ushirikiano wa TACAIDS katika kampeni ya Kili Challenge tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.

“Takwimu za kitaifa za watu wanaoishi na VVU hujuimuisha hata wale wanaoishi Mkoani Geita, ndio maana tunafanya jitihada za pamoja kutokomeza maambukizi mapya nchi nzima,” aliongeza Ndoroma.

GGM Kili Challenge imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli zaidi ya 700 kutoka mabara 6 na zaidi ya nchi 20.

Alisema kampeni hiyo ya GGM Kili challenge ni mojawapo ya majukumu yanayotekelezwa na kampuni hiyo katika kuchangia miradi mbalimbali ya kijamii ambapo kila mwaka hutumia kiasi cha Sh bilioni tisa hadi 11.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu TACAIDS, Dk. Leonard Maboko katika kuhamasisha wananchi kulipa kodi na kutunisha mfuko huo wa mapambano dhidi ya VVU, alisema Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya kodi ambapo sasa wadaiwa au kampuni zinazodaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zinaweza kupata msamaha wa kodi kwa kuchangia mfuko huo.

“Kwa mfano kama kampuni inadaiwa kodi Sh milioni 100, ikitoa Sh milioni 50 kuchangia mfuko wa Ukimwi, itahesabu amelipa kodi hivyo  kule TRA deni lake litabaki milioni 50 pekee,”alisema.

Aliongeza kuwa Serikali imechukua hatua hiyo kwani licha ya mafanikio yaliyofikiwa katika mapambano ya  UKIMWI bado ni tatizo nchini hivyo fedha zinahitajika kutokomeza njanga hilo.

Alisema takwimu zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la maambukizi mapya ya VVU hususan kwa makundi maalum yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi. Hadi kufikia mwaka 2020 idadi ya Watanzania wanaoshi na virusi vya UKIMWI nchini imefikia watu 1,700,000 na Maambukizo mapya kwa mwaka ni watu 68,000.

Alisema kupitia kampeni ya GGM Kilimanjaro challenge, taasisi mbalimbali zimenufaika kwa kupata fedha za kutekeleza shughuli za mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini. Kwa mfano, mwaka 2020 Mfuko wa Kilimanjaro Challenge ulitoa fedha taslim Milioni 800 za Tanzania kwa taasisi 20 zisizo za kiserikali.

Asasi hizo zimetekeleza miradi mbalimbali iliyowalenga vijana, watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, watoto yatima na waliopo kwenye mazingira magumu, na jamii kwa ujumla. Zaidi ya watu 1,000 wamenufaika kutokana na fedha hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles