25.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 28, 2024

Contact us: [email protected]

Gesi asilia itakavyoitajirisha Tanzania

*TPDC yabainisha hatua kwa hatua

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Tanzania inaenda kutajirika na raslimali yake ya gesi asilia. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kuwapo kwa mikakati mizuri iliyofikiwa na Serikali.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) limesema tayari limefikia makubaliano ya awali juu ya ujenzi wa mtambo wa LNG utakaotumika kuchakata gesi asilia kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Ikumbukwe kuwa kukamilika kwa ujenzi wa mitambo hiyo itakuwa ni hatua nzuri kwa Tanzania kuanza kunufaika na raslimali zake kupitia soko la nje.

Wananchi mbalimbali wakiendelea kupata elimu kuhusu miradi inayosimamiwa na TPDC walipotembelea banda hilo katika maonyesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la Serikali ni kuona hadi kufikia Desemba, mwaka huu majadiliano hayo yawe yamekamilika ili iweze kuvuna gesi iliyoko baharini.

“Hadi sasa kiasi cha gesi ambacho tumegundua ni futi za ujazo trilioni 57.54 na kiasi kikubwa kiko baharini ambapo tunatarajia kukivuna ambapo ilikufanikisha hilo tunajenga mtambo wa LNG.

“LNG ni mtambo ambao utachakata hiyo gesi itakayovunwa baharini na kisha itaipooza mpaka ubaridi wa nyuzi joto -160 kisha inasafirishwa kwenda kuuzwa kwenye masoko ya nje, lakini kiasi flani cha hiyo gesi kitabaki nchini kwa ajili ya soko la ndani na Afrika Mashariki na kati.

“Hivyo, hatua tuliyofikia hadi sasa kwa ajili ya kujenga mtambo huo wa LNG ni makubaliano ya awali ambayo nimeyasaini mwezi uliopita mbele ya Rais Samia Suluhu Chamwino jijini Dodoma, hii inamaana kwamba kuna mambo ambayo tayari tumekubaliana kwani lengo letu hadi kufikia Desemba tuwe tumekubaliana mambo yote na tutakuwa tunasaini(HGA) mkataba hodhi wa nchi kabla ya kuingia katika hatua nyingine ya Kiuhandisi na mfumo wa kiwanda kitajengwa vipi,” amesema Dk. Mataragio akizungumzia mkondo huo wa juu.

Picha kwa hisani ya Tovuti ya www.gazetini.co.tz

Akizungumzia Mkondo wa chini, Dk. Mataragio amebainisha kuwa mara baada ya gesi kupoozwa lazima isambaze na kwamba wanajenga miundombinu kwa ajili ya kusambaza gesi majukmbani, viwandani na kwenye magari.

“Katika hilo kwasasa tuna project ya kujenga vituo vitano vya CNG katika maeneo ya Feri, Muhimbili, Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kibaha.

“Hili linakwenda kujibu maswali ambayo yamekuwapo juu ya uhaba wa vituo licha ya unafuu wa gesi asilia uliopo, hii pia itaenda kujenga vituo vingine vidogo,” amesema Dk. Mataragio.

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa TPDC, asilimia 62 ya umeme nchini unatokana na gesi asilia huku kiasi kinachobakia kama asilimia 20 kinatumika katika maeneo ya majumbani na kwenye magari.

“Kiasi hiki ni kikubwa sana ambapo tukisema ukiondoe sehemu kubwa ya nchi itakuwa gizani,hivyo hiki ni kielelezo kwamba hadi sasa Watanzania wanafaidi matunda ya uwepo wa gesi asilia nchini kwao.

“Hivyo, hivyo Watanzania watarajie maendeleo makubwa kwani gesi itakayovunwa mbali na kuzalisha umeme pia itazalisha bidhaa mbalimbali za plastiki pamoja na mbolea hatua ambayo itakuza uchumi ukiachana na fedha itakayopatikana kwa nishati hiyo kuuzwa nje.

“Tunahamasisha pia Sekta Binafsi waje TPDC ili waweze kushiriki katika kujenga vituo vidogo vidogo vya kusambaza gesi asilia ili kuwasaidia watu wenye magari wanaohitaji kuyaunganisha na mfumo wa gesi,”amesema Dk. Mataragio.

Hadi sasa taribani magari 1,500 nchini yameunganishwa na mfumo wa gesi asilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles