24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Gereza kuhamishwa kupisha mgodi  

NA ELIUD NGONDO, MBEYA

GEREZA la Kilimo la Songwe lililoko mjini Mbeya, litahamishwa ili kupisha uchimbaji wa madini ya niobium yaliyopo eneo hilo.

Taarifa hiyo ilitolewa mjini hapa jana na mwakilishi wa Kampuni ya Panda Hill, inayotarajia kuchimba madini hayo, Emmanuel Kisasi.

Kisasi alisema kwamba watahamisha pia nyumba za wafanyakazi wa gereza hilo.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.

“Kwa kuwa eneo lilipo gereza hilo kuna madini, kampuni yetu ya Panda Hill imetenga shilingi bilioni 400 kwa ajili ya kuhamisha gereza hilo, ikiwa ni pamoja na nyumba za watumishi kwa umbali wa kilomita tano.

“Sambamba na hilo, zaidi ya wananchi 467 waliopo maeneo ya mgodi, wanatarajia kunufaika kwa kupata ajira mara tu uchimbaji utakapoanza mwaka 2017.

“Madini hayo tunayotarajia kuyachimba yatatumika kutengeneza vitu vya chuma, kulainisha vyuma na kuwa imara zaidi na pia yanatumika kwenye ujenzi wa nyumba.

“Pia, yatatumika kutengeneza vifaa vya ndege, mabomba ya mafuta, mabomba ya gesi, lensi za kamera pamoja na vifaa vya kompyuta.

“Kwa hiyo, utafiti tulioufanya tumegundua kuna tani milioni 96.3 za madini hayo na yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 30,” alisema Kisasi.

Kwa mujibu wa Kisasi, mgodi huo ni wa nne duniani na kwa Afrika, utakuwa ni wa kwanza kwa kuwa madini hayo hayapatikani kwa urahisi.

Pamoja na hayo, kampuni hiyo ilikabidhi madawati 400 kwa mkuu wa mkoa huo kwa ajili ya kuyasambaza katika shule za msingi saba na sekondari.

Naye Makalla alipokuwa akizungumzia mgodi huo, alisema kuanzishwa kwake kutawanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa kuwa watapata ajira kulingana na uwezo wao.

Alisema pia Serikali itakuwa pamoja na wawekezaji hao ili waweze kufanya kazi kwa mafanikio zaidi ikiwa ni pamoja na kuzingatia taratibu zote za uwekezaji.

Naye Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza, alisema kuwapo kwa mgodi huo, kutawasaidia wananchi wa jimbo lake kubadilika kuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles