23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mabasi ya kampuni ya City Boy yafungiwa

NA YASSIN ISSAH (TSJ), DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limeifungia Kampuni ya City Boy kutoa huduma za usafirishaji nchini kwa   uzembe na kusababisha ajali ambayo watu 30 walifariki dunia wilayani Manyoni Mkoa wa Singida juzi.

Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema Dar es Salaam jana kuwa mabasi hayo, T531 BCE lilokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama na jingine   T247 DCD lililokuwa likitoka  Dar kwenda Kahama, madereva  walikiuka kwa makusudi sheria inayowataka kuendesha kwa mwendo usiozidi kilometa 80 kwa saa.

Juzi, katika  eneo la Miweni-Kintinku mkoani Singida, mabasi mawili ya Kampuni ya City Boy yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu 30 na majeruhi 54.

“Tumeifungia Kampuni ya City Boy kwa  kuhusika katika ajali iliyotokea   Maweni Kintiku.

“Kabla ya ajali hiyo basi moja lilikamatwa Singida mjini likiwa katika mwendokasi wa km 122 kwa saa ambako liliandikiwa faini ya Sh 30,000 na baada ya faini hiyo dereva aliendelea kuendesha kwa uzembe  hadi ajali hiyo ilipotokea,”alisema.

Kutoka Dodoma, Ramadhani Hassan, anaripoti kuwa maiti 13 kati 28  za ajali hiyo  zilizopelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma zimetambuliwa.

Daktari Bingwa wa ajali na Mifupa wa hospitali hiyo,   Dk.Ernest Ibenzi alisema maiti hizo zimetambuliwa na ndugu zao.

Maiti zilizotambuliwa ni pamoja na John Lukanda, Ismail Bashe, Paulo Mfaume, Diocles Wajubigiri, Rabia Levis Lema, Levoso Izrael, Lesta Kanguru Exavely, Kefon Deus.

Wengine ni Paulini Meza, Deogratius Charles Mamunyu, Betty Zumbe, Jesca Lazaro, Leornard Chacha Nyantikela.

Dk. Ibenzi alisema walipokewa majeruhi 15 ambao saba walitibiwa na kurudi nyumbani na wanane wanaendelea na matibabu.

“Wagonjwa wawili tuliowalaza ICU, mmoja hatukumtambua kwani hakuwa na uwezo wa kuzungumza jina lake lakini huyu mwingine tulimtambua kwa jina la Leornard Chacha ambaye amefariki dunia leo (jana).

“Dereva wa moja kati ya magari hayo ambaye alikuwa Manyoni alifariki dunia muda mfupi  baada ya kufikishwa hospitalini,’’ alisema Dk. Ibenzi.

FUNDI: NILIMKANYA DEREVA

Fundi wa gari lililokuwa likitoka Kahama kwenda Dar es Salaam, Salum Mohammed aliliambia MTANZANIA kuwa alimkanya dereva wake kuhusiana na utaratibu wa kusalimia kwa kila mmoja kwenda upande wa mwenzake.

‘’Katika moja ya safari zetu siku zilizopita alifanya hivyo nikamwambia hili litakuja kutugharimu siku moja lakini hakunisikia, sasa ndiyo limetokea wamesababisha vifo hivi,’’alisema Mohammed.

MAJERUHI

Naye majeruhi aliyelazwa wodi namba 11 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mjaidi Waziri mkazi wa Kibaha, alisema wakati ajali  ikitokea alikuwa amelala na aliamka   baada ya kusikia kishindo.

‘’Nilikuwa nimelala nilikuja kushtuka mlio mkubwa wa sauti, siamini kama nimepona ni ajali mbaya sana,’’ alisema.

Monika Rabani Mkazi wa Shelui Mkoani Singida ambaye amelazwa katika wodi namba  8 alisema alikuwa akisafiri  kutoka Dar es Salaam kwenda nyumbani kwao Shelui.

Alisema katika safari hiyo aliongozana na mtoto wa kaka yake aitwaye Mohammed Hassan (2) lakini mpaka wakati huo alikuwa  hajui mtoto huyo yuko wapi.

‘’Sijui mpaka sasa mtoto wa kaka yupo wapi ila ni ajali mbaya sana nimeumia mguu na kuvunjika huu mkono,’’ alisema.

FAMILIA YATEKETEA

Akizungumza katika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Said Musa alisema amempoteza baba yake mdogo, Peter Sinto, mkewe Rose   na mtoto wao ambaye hakukumbuka jina lake.

Alisema Sinto alikuwa akitokea nyumbani kwao Tabora na alikwenda kumtambulisha mkewe Rose   na mwanae baada ya kufunga ndoa mkoani Mbeya hivi karibuni ingawa wazazi walishindwa kuhudhuria ndoa hiyo.

Alisema Sinto alikuwa akirejea katika kituo chake cha kazi cha Mvomero kwa vile  ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mtibwa mkoani Morogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles