Na GUSTAPHU HAULE-PWANI
GARI la Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando (CCM), limekamatwa likiwa limebeba mbao 37 ambazo zilikuwa zinasafirishwa kwa njia ya magendo zikitokea wilayani Kibiti kwenda jijini Dar es Salaam.
Gari hilo aina ya Toyota Landcruser lilikamatwa Januari 2, mwaka huu saa nane jijini Dar es Salaam na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa katika doria likiwa linaendeshwa na dereva Azizi Msumi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Msumi ambaye pia ni dereva wa CCM wilayani Kibiti alikamatwa na mbao hizo huku gari hilo likiwa linapeperusha bendera ya mbunge.
Akizungumza na MTANZANIA jana Ungando, alikiri kukamatwa kwa derava huyo akiwa anaendesha gari yake huku akikanusha kuwa hahusiki na mpango huo na hajamtuma.
Alisema yeye ni mbunge wa CCM na aliombwa gari hilo kwa ajili ya kufanya shughuli za chama lakini hakujua kama linakwenda kusafirisha mbao hizo na ukizingatia hata dereva aliyekuwa analitumia ni wa chama jambo ambalo lilimfanya kutokwa na shaka.
“Hata wewe ndugu mwandishi ebu fikiria, mimi ni mbunge wa CCM na nimeombwa gari na CCM sasa ungekuwa wewe ungefanyaje ? nikaona nisaidie chama changu lakini sikujua yote hayo na kama ningetaka kusafirisha mbao basi ningetumia malori yangu,” alisema Ungando