25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

FIGISU ZATIKISA UCHAGUZI MKUU TUCTA

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA


nicolaus-mgaya

UCHAGUZI wa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) unaofanyika mjini hapa, jana uliingia dosari baada ya wajumbe kuususia.

Wajumbe hao walifikia hatua hiyo kutokana na kile walichosema kuwa hawana imani na kamati iliyokuwa imechaguliwa kusimamia uchaguzi huo.

Hali hiyo nusura ivuruge uchaguzi huo kwa kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wakirushiana maneno ya kashfa, huku wengine wakitoka nje ya ukumbi.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lililazimika kuimarisha ulinzi ili kudhibiti vurugu zilizokuwa na dalili za kutokea.

Hali ya kutoelewana ukumbini ilianza mapema baada ya baadhi ya majina ya wagombea wa nafasi ya rais na katibu mkuu kukatwa katika mazingira yaliyoelezwa kuwa ni yenye utata.

Majina yaliyokatwa kwa upande wa mgombea urais ni Lucas Malunde na Sospeter Omollo na katika nafasi ya katibu mkuu yalikatwa majina ya Saleh Mwasalai na Estomin Kyando.

Wakati majina hayo yakikatwa, yaliyopitishwa katika nafasi ya urais ni Baraka Igangula, Lameck Mahewa, Tumaini Nyamhokya, Raymond Chibuya, Razack Irumba, Dk. Francis Michael na Cosmas Chikoti.

Nafasi ya Katibu Mkuu yalipitishwa majina ya Nicolas Mgaya, Dk. Yahaya Msigwa, Raymond Chibuya, Mponjoli Dickson, Richard Rukambura na Faida Potea.

Katibu wa Tucta, Mkoa wa Dodoma, Ramadhan Mwendwa, alisema mgogoro mkubwa uliokuwa umezuka hadi uchaguzi huo kuchelewa kufanyika, ulitokana na kigezo cha umri wa wagombea.

“Watu wa sekta binafsi walikubali mtu aendelee kugombea hata kama amestaafu, lakini watu wa mashirika ya umma, walitaka mgombea aishie miaka 60. Sasa hapo ndipo mgogoro ulipozuka na wajumbe kuanza kutoiamini kamati ya kusimamia uchaguzi,’’ alisema Mwendwa.

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya, aliiambia MTANZANIA, kwamba kamati ya kusimamia uchaguzi ilivunjwa na kuteuliwa nyingine kutokana na wajumbe kutokuwa na imani nayo.

“Sasa basi, baada ya kamati mpya kuteuliwa, naamini uchaguzi utaendelea kama kawaida kwani lazima tufanye uchaguzi hata kama ni usiku,” alisema Mgaya.

Wakati Mgaya akisema hayo, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kamati ya awali ilikataliwa kwa kuwa haikufuata kanuni za uchaguzi.

“Watu walikuwa na interest zao na walikuwa wakitaka kuweka watu wao, jambo ambalo hatukulikubali,” alisema mjumbe huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles