MSANII wa hip hop, Farid Kubanda (Fid Q), ametamani kuwa na wafuatiliaji wengi katika akaunti yake mpya kama atashindwa kuirudisha akaunti yake ya sasa iliyozuiwa na maharamia wa mtandao.
Akaunti ya msanii huyo kwa sasa inasomeka kwa jina la mrembo wa Tanzania 2007, Wema Sepetu, jambo ambalo linachanganya watu wengi.
“Hawa jamaa wanakatisha tamaa maana mimi nilikuwa natumia mtandao wangu kwa kujitangaza, kutangaza kazi zangu mpya na pia kuwasiliana na wadau wangu mbalimbali, sasa wameharibu kila kitu lakini nitajaribu kurudisha nikishindwa nitaanzisha akaunti mpya, natumaini nitavunja rekodi ya mtoto wa Diamond kwa kupata wafuatiliaji wengi,” alizungumza Fid Q.
Tatizo la mitandao ni kubwa kwa sasa hivyo watu wote wanatakiwa kuwa makini kukagua akaunti zao mara kwa mara.