27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Ferguson anavyowatoa jasho makocha Old Trafford

LONDON, England

TETESI zilikuwa nyingi lakini wikiendi iliyopita zikawa stori kamili baada ya Manchester United kumfukuza kwenye benchi la ufundi kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer.

Solskjaer aliyesaini mkataba mpya wa miaka mitatu miezi mitano iliyopita, alifutwa kazi baada ya kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Watford, kikiwa ni kichapo cha tano katika mechi saba za Ligi Kuu walizocheza hivi karibuni.

Hata hivyo, Solskjaer anakuwa kocha wa nne kutimuliwa na Man United tangu Alex Ferguson alipostaafu miaka saba iliyopita. Kwamba Solskjaer anaungana na David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho ambao kwa nyakati tofauti walijaribu bila mafanikio kuvaa viatu vya lejendari huyo.

Alivyowapiga bao Moyes, Mourinho

Cha kushangaza zaidi, Solskjaer asiye na uzoefu mkubwa kwenye ukocha, amezidiwa na Mourinho tu linapokuja suala la takwimu za idadi ya mechi za kushinda. Kati ya wanne hao, Mourinho ndiye aliyekuwa ameshinda mechi nyingi (58%) na sasa Solskjaer anashika nafasi ya pili (54%), akifuatiwa na Moyes (53%) na Van Gaal (52%).

Pia, rekodi ya Solskjaer kushinda asilimia 39 ya mechi alizokutana na vigogo (Manchester City, Liverpool, Chelsea, Arsenal na Tottenham) ni nzuri, ukilinganisha na Moyes na Mourinho, ingawa anazidiwa na Van Gaal.

Katika mechi 36, Solskjaer alishinda 14, alifungwa 12 na kuondoka na sare 10. Van Gaal alikutana na vigogo hao mara 23 na kushinda mechi 10, sawa na ushindi wa asilimia 43.

Kingine Solskajer alichowaacha mbali makocha watatu waliomtangulia ni matumizi kwenye soko la usajili. Ameondoka akiwa ‘ameshatumbua’ Pauni milioni 441 (zaidi ya Sh tril. 1.3 za Tanzania), kiasi kikubwa zaidi mbele ya walichotumia Mourinho (Pauni mil. 430.8), Van Gaal (Pauni mil. 309.2), na Moyes (Pauni mil. 69).

Alivyotia aibu, Old Trafford ‘shamba la bibi’

Solskjaer ameondoka Man United akiwa kocha wa kwanza tangu mwaka 1895 kuifanya timu hiyo ifungwe mabao 5-0 na Liverpool ikiwa nyumbani, Old Trafford. Ikawa mara ya kwanza tangu mwaka 1995 kuiona Man United iliyoko Old Trafford ikiruhusu mabao matano bila kupata bao.

Chini ya kocha huyo raia wa Norway, Old Trafford ikapoteza heshima yake, hata kufikia hatua ya Burnley kuondoka na ushindi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1962, huku Sheffield United nao wakizoa pointi tatu uwanjani hapo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1973.

Kwa upande mwingine, Solskjaer ametimuliwa akiwa hajaipa taji lolote Man United, wakati Mourinho aliipa Man United ‘ndoo’ ya Ligi ya Europa na Kombe la Ligi, huku Van Gaal akifanikiwa kulifungia kabatani Kombe la FA.

Juu ya ukame wa mataji, Solskjaer hana tofauti na Moyes aliyefukuzwa akiwa ameinoa Man United kwa miezi 10 tu, ambapo aliifanya timu hiyo imalize nje ya top four kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995.

Nani anafuata?

Kuna orodha ndefu ya makocha wanaohusishwa na kiti kilichoachwa na Solskjaer pale Old Traford. Zinedine Zidane hana kazi tangu alipoondoka Real Madrid. Mwingine ni Brendan Rodgers wa Leicester City.

Wakati huo huo, Erik ten Hag anayeinoa Ajax naye ahatajwa kwenye mitaa ya jijini Manchester. Ni kama ilivyo pia kwa mkuu wa benchi la ufundi la PSG, Mauricio Pochettino.

Je, nani ataingia kwenye kitanzi kilichowanyonga Moyes, Van Gaal, Mourinho na Solskjaer? Ni suala la kusubiri na kuona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles