Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais Samia Suluhu Hassan, leo Julai mosi, 2021 amepokea taarifa ya Ukaguzi Maalum kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayohusu matumizi ya fedha zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kati ya Januari na Machi mwaka huu.
Taarifa hiyo inatokana na agizo alilolitoa Rais Samia Machi 28, 2021, wakati akipokea Taarifa ya CAG kwa mwaka 2019/ 2020.
Katika taarifa ya ukaguzi maalum, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Charles Kichere amesema katika ukaguzi uliofanyika imebainika kuwa fedha zilizotolewa BoT katika kipindi hicho zilifuata taratibu zote, isipokuwa baadhi ya malipo yaliyokuwa yanatoka Hazina Kuu kwenda katika Taasisi mbalimbali za serikali yalibainika kuwa na mapungufu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mapungufu hayo ni pamoja na baadhi ya taasisi kama vile Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mamlaka ya Bandali Tanzania (TPA), kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika.
Vilevile, CAG Kichere amesema yamejitokeza mapungufu ambapo baadhi ya Makandarasi waliotoa huduma kucheleweshewa malipo yao hali iliyosababisha madeni ya makandarasi kuwa makubwa kutokana na riba ambayo ni mzigo kwa serikali.
Mapungufu mengine ni pamoja na kuwepo kwa Miradi ambayo haikupangwa na hivyo kufanya Malipo nje ya bajeti ya serikali.