23.2 C
Dar es Salaam
Friday, June 9, 2023

Contact us: [email protected]

Bashe aagiza Halmashauri kuwezesha vikundi vya wakulima

Na Allan Vicent, Tabora

Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wametakiwa kutumia asilimia 10 za mapato yao ya ndani kuwezesha vikundi vya wananchi wanaojishughulisha na shughuli za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuwainua kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa Juni 30, 2021 na Naibu Waziri wa Kilimo, Husein Bashe alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani (SUDU) yanayofanyika Kitaifa mkoani Tabora.

Amesema dhamira ya serikali ni kujenga taifa la wazalishaji hivyo ipo haja kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha asilimia 10 inayotengwa kuwezesha wananchi kiuchumi inapelekwa kwenye vikundi vya wakulima.

Amebainisha kuwa sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 26 ya pato la taifa, hivyo kama wakulima watawezeshwa wanaweza kuongeza kasi ya uzalishaji mazao mbalimbali hivyo kuwezesha serikali kuwa na chakula cha kutosha.

Amefafanua kuwa mazao ya kimkakati ya pamba, korosho, alizeti, tumbaku na kahawa ambayo yamekuwa yakisisitizwa na serikali, kama yatasimamiwa ipasavyo yanaweza kuingiza zaidi ya sh Trilioni 5 kwa mwaka hivyo kuwainua wakulima.

Bashe alisisitiza kuwa ili kuhakikisha sekta ya kilimo inaleta tija kwa uchumi wa nchi, serikali imekuwa ikiwezesha vyama vya ushirika ili viweze kuwa na nguvu na uwezo wa kushindana na sekta binafsi nyingine.

“Dhamira ya serikali ni kuwasaidia wakulima kupitia vyama vya ushirika, hivyo kinachotakiwa ni kujipanga vizuri na kuongeza mazao mengine, jambo la msingi ni pamoja na vikundi kushirikiana na wadau wengine ili kufikia malengo.

“Kuanzia sasa badala ya mkulima kwenda benki kukopa fedha za pembejeo na kulipa kwa riba, Msambazaji atapeleka pembejeo kwa mkulima moja kwa moja na atalipwa baada ya mavuno kukamilika,” amesema Bashe.

Alisisitiza kuwa wakulima wanaaminika tatizo lipo kwa viongozi wao, hivyo akawataka kusimamia makubaliano yaliyofikiwa huku akiwahakikishia kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao ili kujenga ushirika wenye nguvu.

Ili kuhakikisha Maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani inaleta tija kubwa kwa wakulima, ameagiza kuwa yatakuwa yanafanyika katika eneo moja kwa miaka mitatu mfululizo kabla ya kuhamia mkoa mwingine.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Dk. Benson Ndiege amesema ushirika ni nyenzo muhimu ya kuinua wananchi wenye vipato vidogo kiuchumi, hivyo akashauri kusimamiwa ipasavyo ili uwe imara zaidi.

Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustin Kamuzora alisema maendeleo ya ushirika ni maendeleo ya wananchi hivyo akashauri wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza mambo mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,351FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles