26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Fedha, simu za mkononi husababisha kuhara

MWANDISHI WETU

UTAFITI mpya umeonya kuwa fedha chafu na simu za mkononi zinaweza kuwa na hatari kubwa kwa afya ya mwanadamu.

Kwa mujibu wa wanasayansi, fedha hususani zile zenye thamani ndogo, yaani zinazopitia mikononi mwa watu wengi zaidi, zinasababisha magonjwa mengi ya kuhara.

Husababisha maradhi hayo miongoni mwa watu wanaotumia chakula kinachoandaliwa kwenye maeneo ya hoteli, migahawa na vilabu.

Utafiti huo ulishirikisha waandaaji wa vyakula 395 katika maeneo 15 tofauti ya jiji la Nairobi na kuendeshwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Jomo Kenyatta na kile cha teknolojia nchini humo (JKUAT).

Ulifanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Tiba Kenya (Kemri), na Kitengo cha Utafiti wa Matibabu cha Jeshi la Marekani nchini humo.

Utafiti huo ulionyesha kwamba kwasababu fedha na simu za mkononi huwa hazisafishwi, hugeuka kuwa maficho ya vimelea vingi vya magonjwa ambao husababisha sumu kwenye vyakula hivyo.

Baada ya kuchunguza sarafu kuanzia ya shilingi moja hadi noti za Sh 1,000 zinazotumiwa jijini Nairobi, ripoti ilifichua kuwa sarafu za Sh 5, 10, 20 ndizo zilizokuwa chafu zaidi zikifuatiwa na noti za Sh 50, 100 na 200.

“Nyingi kati ya fedha pamoja na simu zilikuwa na bakteria wanaosababisha magonjwa ,” matokeo ya utafiti huo yanabainisha.

Matokeo hayo yalikuwa yamewasilishwa katika mkutano wa saba wa Afya na Sayansi wa Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, Machi mwaka huu.

Mbaya zaidi, wahudumu wa vyakula, hususan wanaogawa vyakula kwa wateja pamoja na wapishi ilibainika kuwa huwa hawazingatii kanuni za usafi hasa baada ya kupokea simu zao za mkononi.

Wakati wa utafiti huo, washiriki 34 miongoni mwa wale wanaoandaa vyakula walikutwa na magonjwa kama vile kikohozi, kichomi na maumivu ya tumbo na utumbo (gastroenteritis).

Magonjwa hayasababishi matatizo tu, bali pia yanaweza kuambikizwa kutoka mwandaaji wa chakula, anayegawa chakula au mpishi wa chakula anayeumwa kwenda kwa mteja.

Aidha, ilibainika kuwa asilimia 60 ya waliofanyiwa utafiti hawakuwa wamenawa mikono yao baada ya kupokea simu zao za mikononi.

Kwa kawaida, waandaaji wa chakula hawapaswi kupokea simu.

“Wanaoshughulikia chakula na umma kwa ujumla hawanabudi kuhamasishwa juu ya hatari zinazoweza kutokea kutokana na kugawa chakula baada ya kushika fedha au simu za mkononi,” ulionya utafiti huo.

Mwaka 2009, Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini Kenya (Kemri) ilifanya utafiti sawa na huo jijini Nairobi na kugundua kuwa simu za mkononi zina vimelea wa magonjwa kwa kiasi kikubwa na baadhi zikiwa hata va vimelea wanaopatikana kwenye kinyesi.

Nyingi kati ya fedha zilizopatikana na vimelea zilikuwa ni sarafu zilizochukuliwa kutoka kwenye machinjio.

Zilifuatiwa na zile zilizokusanywa kutoka kwa wauzaji wa mahindi wa kando ya barabara na vyakula vinavyouzwa kwenye maduka madogo (vioski).

Kwa mujibu wa Dk. Richard Korir, Ofisa wa Utafiti katika Kituo cha Kitengo cha Utafiti wa Mikrobiologia na mwandishi wa utafiti huo, kutofuatwa kwa kanuni ya kuosha mikono na usafi kwa ujumla kunasababisha kuhamishwa kwa vimelea hawa wa magonjwa kwenye chakula ambacho bila shaka kinaliwa.

Utafiti huo ulifanywa na kuwasilishwa na mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kilimo (JKUAT) ambaye aliangazia aina mbalimbali za bakteria wanapatikana katika mazingira, chakula, utumbo na ngozi katika wanyama na binadamu.

Ingawa vimelea vingi vya bakteria hawa si hatari, baadhi wanaweza kusababisha magonjwa kama vile homa ya matumbo, sumu ya chakula na maambukizi ya ngozi.

“Shilingi 1,000 ndiyo yenye maambukizi ya chini kwa sababu hutumiwa mara chache, huku sarafu ya shilingi moja ikiwa pia haina uchafu mwingi na thamani yake imeshuka kwa hiyo haitumiwi mara nyingi,” anabainisha Dk. Korir.

Vimelea waliopatikana zaidi walikuwa ni wa jamii ya staphylococcus, wanaofahamika kwa kusababisha maambukizi ya ngozi, moyo na mifupa, sumu ya chakula, kichomi na sumu ya mwili wa binadamu.

Bakteria waliopatikana katika chakula pia ni jamii ya Escherichia coli (E. coli), ambao hupatikana katika mazingira, chakula na utumbo wa binadamu na wanyama.

Wengi kati ya vimelea hao si hatari lakini wanaweza kukufanya uwe mgonjwa.

Jambo la kushangaza ni kwamba, D.i Korir anasema, zikilinganishwa na fedha, simu za mkononi ni mbaya zaidi linapokuja suala la maambukizi ya magonjwa.

“Watu wengi hawadhani kuwa simu ni chafu au ni chanzo cha kuambukizwa magonjwa kwa hiyo, mara nyingi hawazingatii usafi baada ya kuzitumia,” anasema.

Simu ziligundulika kuwa bakteria 12 baada ya kukusanywa na kuchunguzwa na zaidi bakteria aina ya Staphylococcus, ambao mara nyingi hupatikana katika nywele na ngozi.

Makala haya yameandaliwa na Mwandishi Wetu kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles