28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Habari feki chanzo ugumu kutokomeza Ebola DRC

HASSAN DAUDI Na MITANDAO

UGONJWA wa Ebola umeendelea kuitikisa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa miezi kadhaa sasa, safari hii hali ikielezwa kuwa mbaya zaidi katika historia ya ugonjwa huo nchini humo.

Watu zaidi ya 970 wameshapoteza maisha, huku maambukizi mapya yakitajwa kufikia 1,400 tangu Agosti, mwaka jana. Hatari zaidi imekuja baada ya wataalamu wa afya kubaini kuwa asilimia 90 ya watu wanaopata maambukizi hupoteza maisha.

Wakati juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zikiendelea kwa msaada mkubwa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inaelezwa kuwa kumekuwapo changamoto ya habari za uongo (fake news) katika vita ya kuutokomeza ugonjwa huo.

“Taraifa za upotoshaji zimekuwa zikienezwa kupitia makundi ya Facebook, WhatsApp, jumbe zikitumwa kwa Lugha ya Kifaransa, Kiswahili au Kinande (inayozungumzwa DRC),” inasema taarifa ya mtandao wa Congo Check.

Hivi sasa, nguvu kubwa inafanywa na Shirika la Watoto la Kimataifa (UNICEF) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya nchini DRC, wakipambana kukabiliana na habari za uzushi, ambazo nyingi zimetengeza hofu kwa wananchi.

Kutokana na uzushi unaodai ugonjwa huo hautibiki, wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipuuzia kwenda hospitali. Hilo limesababisha wengi kutokuwa na imani na mikakati ya kuuondoa ugonjwa huo DRC.

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana, mwanasiasa wa upinzani, Crispin Mbindule Mitono, aliibua madai kuwa Serikali ya DRC ndiyo iliyotengeneza kirusi cha Ebola.

Katika mahojiano yake na kituo cha redio, alisema lengo ni kupunguza idadi ya wananchi katika Jiji la Beni, ambalo ndio la kwanza kuvamiwa na ugonjwa huo.

Ukiacha hilo, wananchi walikuwa wakizidishiwa hofu na taarifa za mitandaoni kuwa miili ya waliofariki kwa Ebola ilikuwa ikiibwa na kwenda kutolewa viungo, ambavyo mwishowe vilikuwa vikiuzwa.

“Huwa naiambia timu yangu kwamba tunapambana na matatizo mawili, Ebola na hofu (inayotokana na habari za uongo),” anasema mmoja kati ya viongozi kutoka UNICEF, Carlos Navarro Colorado.

Wakati huo huo, wapo wananchi wanaoamini timu ya madaktari wa Ebola ndiyo inayoeneza virusi hivyo katika makazi ya watu kwa kupulizia vyooni na bafuni, wengine wakisema huenezwa kwa kutumia helikopta.

Lakini pia, bado umekuwapo uvumi kuwa hakuna Ebola nchini humo, tafiti zikionesha kuwa kati ya watu wanne nchini DRC, mmoja anaamini hivyo.

“Hakuna kitu kama hicho kiitwacho Ebola. Ni uzushi wa serikali tu,” anaandika mmoja kati ya watumiaji wa mtandao wa Facebook.

Ripoti ya Chuo Kikuu cha Harvard ilionesha kuwa kati ya watu 961 wa miji ya Beni na Butembo, ni 340 pekee waliokuwa wakiamini uwapo wa Ebola, huku wengine 230 wakisema ni tetesi tu na hakuna kitu kama hicho.

Aidha, watafiti wa taasisi hiyo ya elimu ya juu walibaini kuwa wasioamini kuwa Ebola ipo nchini DRC ni wale wanaodai kuibuka kwa ugonjwa huo ni uzushi ulioandaliwa na wajanja wachache ili kujiingizia kipato, ukiacha waliouchukulia kuwa ni ajenda ya kisiasa tu.

Kujaribu kukabiliana na upotoshaji wa aina hiyo, Mkurugenzi wa kampeni ya kutokomeza Ebola kutoka WHO, Michael Ryan, anasema kupitia mitandao ya kijamii wamefanikiwa kwa kiasi fulani kueneza elimu kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya taarifa za upotoshaji.

“Tumeweza kuzifanya jamii zitenganishe jitihada za kuzuia Ebola na ajenda za kisiasa. Hiyo imesaidia,” anasema Ryan.

Pia Serikali ya DRC imeajiri vijana waliopewa kazi ya kuzifikisha mezani taarifa zote za upotoshaji zinazojitokeza katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, ambao ndiyo wenye watumiaji wengi nchini DRC, hii ni kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Afya, Jessica Ilunga.

Si tu kutoa elimu, pia familia zimekuwa zikiruhusiwa kushuhudia maziko ya ndugu zao waliofariki kwa ugonjwa huo, japo hilo limekuwa likifanywa kwa tahadhari kubwa ili kudhibiti maambukizi.

Hali hii ni tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wakitakiwa kukaa mbali au hata kutoruhusiwa kabisa kuwaona wagonjwa, ikikumbukwa kuwa hata shughuli za mazishi hazikuwa zikiwashirikisha wananchi.

“Tulichojifunza ni kwamba hatutakiwi kubadilisha chochote katika taratibu za kimila katika mazishi. Tunachotakiwa kukifanya ni kuhakikisha tunalinda usalama wa afya za waombolezaji tu,” anasema Mtaalamu wa Sayansi ya Tamaduni, Juliet Bedford.

Hata hivyo, wakati hilo la taarifa za upotoshaji likionekana kuwa kikwazo, ipo pia hoja ya kutokuwapo kwa hali ya utulivu katika maeneo mbalimbali ya DRC.

Mathalan, ukiitazama Kivu Kaskazini, bado kumekuwapo na machafuko ya mara kwa mara kutokana na uwapo wa vikundi vya waasi. Ni changamoto kubwa kwa madaktari kufika, ikizingatiwa kuwa wapo walioshambuliwa wakiwa huko.

Ni maeneo hayo ndiko katika miaka ya hivi karibuni, vituo vya tiba za Ebola vimekuwa vikivamiwa na huku madaktari wakipoteza maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles