KINSHASA, DRC
MSHINDI wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu nchini hapa, Martin Fayulu, juzi aliwasilisha rasmi pingamizi katika Mahakama ya Katiba kuyakataa matokeo ya uchaguzi akisema yalighubikwa na udanganyifu.
Fayulu alisema matokeo ya uchaguzi wa Desemba 30 yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CENI, yalikuwa yamepangwa na ametoa wito kura zihesabiwa upya.
Mahakama ya Katiba ina siku saba za kuisikiliza rufaa hiyo.
Fayulu anayapinga matokeo ya uchaguzi wa Desemba 30 mwaka jana yaliyompa ushindi Felix Tshisekedi ambaye pia ni kutoka upande wa upinzani.
Alisema Tshisekedi alishinda uchaguzi huo kutokana na mpango wa siri uliofikiwa kati yake na Rais anayeondoka madarakani, Joseph Kabila.
Muungano wa vyama vya upinzani unaoongozwa na Fayulu na unaojulikana kama Lamuka, unadai kiongozi wao alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 61, hiyo ikiwa ni kulingana na waangalizi 40,000 wa uchaguzi kutoka Kanisa Katoliki.
CENI ilisema Fayulu alipata asilimia 34 ya kura zilizohesabiwa huku Tshisekedi akishinda kwa kupata asilimia 38.
Fayulu aliwaambia waandishi habari kwamba miongoni mwa mambo anayotaka ni pamoja na kubandikwa karatasi za matokeo nje ya vituo vya kupigia kura.
Toussaint Ekombe, wakili wa Fayulu alisema kiongozi huyo anataka yafutwe matokeo ya awali yaliyotangazwa na CENI na kumpa Tshisekedi ushindi.
Akizungumza juzi na waandishi habari nje ya mahakama hiyo, Ekombe alisema rufaa hiyo iliwasilishwa Ijumaa.
Fayulu alisema anaamini Mwenyekiti wa CENI, Corneille Nangaa alikiuka sheria ya uchaguzi wa Desemba 30 mwaka jana katika kumchagua mrithi wa Rais Kabila.
Hata hivyo, Nangaa alisema kuna njia mbili tu za kuzichukua hivi sasa: moja ni kuyakubali matokeo rasmi ya uchaguzi au kufutwa uchaguzi huo na kuendelea kumuweka madarakani Rais Kabila hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.
”Wananiita mimi ni askari wa watu na sitowaangusha watu wangu,” alisema Fayulu. Alisema kuwa pingamizi aliloliwasilisha mahakamani linajumuisha ushahidi kutoka kwa mashahidi waliokuwapo kwenye vituo vya kupigia kura.
Katika hatua nyingine, vikosi vya usalama nchini hapa viliyazingira makazi ya Fayulu na kwenye mahakama alikokuwa akitarajiwa kwenda kuwasilisha pingamizi la kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo.
Watu walioshuhudia walisema wanajeshi na polisi waliyazingira maeneo hayo kabla Fayulu hajawasilisha pingamizi lake mahakamani.
Wafuasi kadhaa wa Fayulu waliokusanyika nje ya hoteli yake mjini hapa pamoja na makazi yake, walikuwa wakiimba nyimbo za kumpinga Rais Kabila pamoja na Rais mteule, Tshisekedi, huku wakihisi kwamba kuzingirwa kwa maeneo hayo ni jaribio la kumtisha Fayulu.
Hayo yalitokea wakati muungano wa vyama vinavyoiunda serikali inayoondoka madarakani umepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wabunge. Matokeo hayo yalitangazwa juzi alfajiri na CENI.