28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Fatma Karume aja na hoja mpya wakurungenzi, uchaguzi

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

WAKATI sakata la wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya, miji na majiji kusimamia uchaguzi likiendelea kushika kasi, Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, amesema hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda wa Dar es Salaam haijawapiga marufuku viongozi hao kusimamia uchaguzi wa madiwani.

Akizungumza na MTANZANIA JUMAPILI, Fatma alisema wakurugenzi hao hawajapigwa marufuku kwa sababu uchaguzi wa madiwani unafanyika chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa  tofauti na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inayosimamia uchaguzi wa rais na wabunge  ambayo ndiyo Mahakama Kuu ilipiga wateule hao wa Rais kusimamia.

Kauli hiyo ya Fatma imekuja siku chache baada ya Juni 2 mwaka huu vyama vinane vya upinzani kutishia kutoshiriki uchaguzi wa marudio katika kata 32 unaotarajiwa kufanyika Juni 15 endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hakitatekeleza hukumu hiyo ya Mahakama.

Akifafanua katika hilo, Fatma alisema kuna sheria mbili zinazosimamia chaguzi nchini ikiwamo Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inayosimamia uchaguzi wa Rais na wabunge na pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo inahusu uchaguzi wa madiwani na viongozi wengine wa serikali za mitaa.

“Uamuzi wa Mahakama Kuu umelenga uchaguzi wa Rais na wabunge kwa sababu wao hawachaguliwi chini ya National Election Act (Sheria ya Taifa ya Uchaguzi), hawa wengine wanachaguliwa chini ya Local Election Act (Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa). 

“Sasa Local Election Act bado haijapigwa marufuku. Kile kifungu kinachoruhusu ma-DED kuwa wasisimizi wa uchaguzi kwenye Local Election Act hakijapigwa marufuku kwenye National Election Act Mahakama imeshapiga marufuku kile kifungu.

“Tatizo ni hivi, kwamba serikali kwa sababu Mahakama Kuu imeshasema kwamba ile sheria ya National Election Act haifuati Katiba, ina wajibu wa kutazama sheria zote nyingine zilizokuwa kama hii ili izibadilishe bila watu kwenda mahakamani. Huo ndiyo wajibu wa Serikali,” alisema Fatma.

Kuhusu kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, kuwa baada tu ya serikali kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 10 mwaka huu kuwazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi, kwamba utekelezaji wa hukumu hiyo unasimama hadi pale rufaa ya serikali itakapoamriwa, Fatma alisema kusudio hilo halizuii kutekelezwa kwa hukumu hiyo.

“Haizuii kabisa hukumu ya Mahakama kutekelezwa, hukumu ya Mahakama haiwezi kuachwa kutekelezwa kwa sababu Kilangi kakata rufaa. Lakini vilevile hii kesi haijahusu local election (Uchaguzi wa Serikali za mitaa)  inahusu National election (uchaguzi wa kitaifa).

“Uchaguzi unafanyika chini ya sheria tofauti, hata kama unafanyika siku moja lakini unafanyika kwa sheria tofauti. Ni kama Zanzibar kuna chaguzi kama tatu hivi zinafanyika siku moja, unafanyika uchaguzi wa Rais na Baraza la wawakilishi Zanzibar chini ya sheria nyingine, uchaguzi wa madiwani sheria nyingine na uchaguzi wa wabunge na Rais wa Tanzania kwa sheria nyingine,” alisema Fatuma.

HUKUMU YA MAHAKAMA KUU

Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, aliyekuwa akitetewa na Wakili Fatma Karume, pia Mahakama hiyo ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Mahakama ilidai vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao huteuliwa na rais aliyeko madarakani, ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Pia ilisema sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake.

Jaji Ngwala, alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, kifungu namba 7(1) na 7(3) ni batili kwa sababu kinatoa nafasi kwa wateule wa Rais ambao pia si waajiriwa wa NEC kusimamia uchaguzi.

Alisema kifungu cha 7(1) kinasema kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na sheria mama ambayo inasimamia nchi. Pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Jaji Ngwala alisema lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote anayekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Alisema kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa waleta maombi, vimeonyesha pasi na shaka kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana masilahi na wateule wao.

Kutokana na hali hiyo, alisema mahakama imeona kuwa vifungu hivyo ni batili na kwamba havifai kutumika wakati wa kusimamia uchaguzi.

Hata hivyo Mei 13 Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, alisema serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi kwa niaba ya (NEC).

Dk. Kilangi alisema tayari Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG) imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Alisema kuwapo kwa hukumu hiyo hakuathiri chaguzi nyingine zijazo zikiwemo za marudio, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamriwa.

MSIMAMO WA UPINZANI

Juni 2 mwaka huu vyama vinane vya upinzani vilitishia kutoshiriki uchaguzi wa marudio katika kata 32 unaotarajiwa kufanyika Juni 15 endapo NEC hakitatekeleza hukumu hiyo ya Mahakama.

Vyama vilivyosusia ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi,Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), UPDP, NLD,CCK na DP.

Viongozi hao walisema kitendo cha NEC kuwaruhusu wakurugenzi kuendelea kusimamia uchaguzi huo wa marudio ni kuidharau Mahakama na kwamba hata vyama vyao haviwezi kushiriki kwa kuwa kufanya hivyo ni kushiriki katika dharau dhidi ya hukumu ya Mahakama.

KAULI YA NEC

Hata hivyo Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Athuman Kihamia, aliliambia gazeti moja la kila siku kuwa uchaguzi huo wa madiwani hauathiri kwa namna yoyote hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na kwamba haujavunja matakwa ya hukumu hiyo wala haungiliani.

“Tume inaheshimu maamuzi ya Mahakama Kuu na inawahakikishia kuwa haijagusa au kuathiri sehemu ya vifungu ambavyo Mahakama Kuu imevitolea hukumu,” alisema Dk. Kihamia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles