Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam
FAMILIA ya bilionea Erasto Msuya, imeibua mapya mahakamani baada ya kuwasilisha barua ya kumkataa hakimu anayesikiliza kesi ya mauaji ya binti yao, marehemu, Aneth Msuya.
Familia hiyo miliwasilisha barua katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa anayesikiliza kesi hiyo.
Katika kesi ya mauaji, mke wa bilionea Msuya, Miriam Msuya na mfanyabiashara, Revocatus Muyela, wote wakazi wa Arusha, wanatuhumiwa kumuua dada wa bilionea Msuya, Aneth.
Washtakiwa hao jana walipanda kizimbani mbele ya Mwambapa, wakati kesi yao ilipokuja  kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa kuwaachia ama laa kutokana na maombi yaliyowasilishwa na wakili wa utetezi, John Mallya.
Wakili Mallya, aliwasilisha ombi hilo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuiomba mahakama iwape muda ili watekeleze amri hiyo iliyowataka wabadilishe hati ya mashtaka.
Mallya, alidai amri ya mahakama ni sheria na kama hawatekelezi sheria hiyo, hakuna hati yoyote inayowashikilia washtakiwa hao, hivyo aliomba waachiwe huru.
Kishenyi alidai hawajakataa kutekeleza amri ya mahakama, lakini wanaomba muda, pia wanaweza kuiarifu mahakama kama wanakata rufaa au laa.
Aliiomba mahakama isikubali ombi la washtakiwa, bali iendelee kuwashikilia kwa mujibu wa sheria.
Mallya aliomba mahakama kuwaachia huru washtakiwa kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kutekeleza amri ya mahakama, iliyowataka kuifanyia mabadiliko hati ya mashtaka kwa kuwa inamakosa.
Kabla ya kutoa uamuzi, Hakimu Mwambapa alisema hawezi kutoa uamuzi kwa kuwa anasubiri maelekezo kutokana na barua iliyowasilishwa mahakamani hapo.
Akizungumzia barua hiyo, alisema inatoka familia ya marehemu Simon Msuya.
Alisema hataweza kutoa uamuzi na kuiahirisha kesi hiyo hadi Februari 6, mwaka huu, kwa kutajwa na washtakiwa walirudishwa rumande.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo, familia ya marehemu Aneth imeandika barua na kuiwasilisha mahakamani hapo kueleza hawana imani na Hakimu Mwambapa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa Mei 25, mwaka jana, maeneo ya Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, walimuua Aneth.