22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AIOMBA UTURUKI UJENZI RELI YA KATI

Na Mwandishi Wetu


Rais Dk. John Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, wakiwasalimia wananchi waliofika kwenye mapokekzi ya mgeni huyo katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam jana.
Rais Dk. John Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, wakiwasalimia wananchi waliofika kwenye mapokekzi ya mgeni huyo katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Dk. John Magufuli amesema Rais wa Uturuki, Tayyip Erdogan, ameonesha nia kwa Serikali yake kuisaidi Tanzania kupata mkopo kupitia Benki ya Exim ya nchini mwake, utakaotumika kujenga reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge).

Alisema mojawapo ya kampuni zilizoomba zabuni ya kujenga reli hiyo ni kutoka Uturuki, hivyo amemwomba Rais Erdogan kuwa endapo itashinda zabuni, Exim itoe mkopo kwa ujenzi wa sehemu ya reli hiyo ambayo ina urefu wa zaidi ya kilomita 400.

Akizungunza Dar es Salaam jana wakati wa kusaini mikataba tisa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki, Rais Magufuli alisema kati ya mambo mengi waliyozungumza katika mazungunzo yao ya faragha, ni pamoja na suala la ujenzi wa reli hiyo inayoiunganisha Tanzania na nchi jirani, zikiwamo Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Tumezungumza mambo mengi sana, nikamwomba atusaidie Benki ya Exim ya Uturuki itukopeshe hela za kujenga eneo moja la reli yetu kwa ‘Standard Gauge’ akakubali na kusema atatoa maelekezo kwa watu wake, aliniuliza ni umbali gani nikamwambia ni kilometa 400, akasema hiyo ni kidogo sana,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema pia nchi ya Uturuki ni ya saba kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, hivyo uhusiano unaoendelea kujengwa na nchi hizo mbili utazinufaisha zaidi katika sekta hiyo.

Alisema mahusiano ya nchi mbili hizi kwenye sekta ya ulinzi yataisaidia Tanzania zaidi kwenye mafunzo.

Baada ya shughuli ya kusaini mikataba hiyo kumalizika na viongozi hao kuzungumza na vyombo vya habari, Rais Magufuli alipanda gari la Rais Erdogan lililokuwa pia na nembo yake tofauti na ile ya ‘Bibi na Bwana’ inayotumiwa na Rais wa Tanzania na kwenda naye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kulikokuwa kumepangwa kufanyika mkutano wa viongozi hao na wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliwataka wafanyabiashara wa Uturuki kuchangamkia fursa za uwekezaji, hasa kilimo hapa nchini kwani kati ya hekta milioni 44 za kilimo, zilizoendelezwa hadi sasa ni takribani milioni 10.

Aliwataka pia wafanyabiashara wa Tanzania kubadilishana mawasiliano na wenzao wa Uturuki ili kuweza kufanya biashara kwa siku za usoni.

Kwa upande wake, Rais Erdogan aliahidi kushirikiana na Tanzania kukuza uwekezaji na biashara.

Alisisitiza umuhimu wa kukuza kiwango cha biashara angalau kifikie Dola milioni 500 kwa mwaka.

Rais Erdogan pia alielezea tukio la jaribio la uhaini dhidi ya Serikali yake lililofanywa na kikundi cha Fethulla Julai 15, mwaka 2016 ambalo lilisababisha vifo vya watu 240 na maelfu ya majeruhi nchini humo.

Alisema wafuasi wa kikundi hicho kilichopanga jaribio hilo wamesambaa hadi katika nchi za Afrika, hivyo aliomba viongozi wa nchi za Afrika kushirikiana naye katika kukabiliana nao ili kujihakikishia amani kwa maendeleo ya kiuchumi.

Alihitimisha mazungumzo yake kwa kumwomba Rais Magufuli azuru nchini Uturuki wakati wa ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo. Prof. Elizabeth Kiondo aliteuliwa kuwa balozi wa kwanza.

“Tumeona kuna fursa kubwa ya kushirikiana kwenye kilimo, reli na ujenzi na tunalenga kuyakuza haya,” alisema Erdogan.

Alisema kwa sasa biashara kati ya mataifa hayo mawili ni Dola za Marekani milioni 150, lakini inaweza kupanda hadi kufikia Dola za Marekani milioni 500.

Mikataba iliyosainiwa kwenye shughuli hiyo ni ule wa ushirikiano kati ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na lile la Uturuki (THY), Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) na lile la Uturuki (TRT), ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili, elimu na utafiti, ushirikino kati ya Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo Tanzania (Sido) na lile la Uturuki pamoja na ushirikiano kwenye sekta ya utalii.

Mingine ni ile ya ushirikiano kwenye viwanda vya ulinzi, afya na Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na kile cha Uturuki.

Akizungumzia mafanikio ya ziara hiyo ya Rais Erdogan, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema mkataba wa sekta ya afya uliosainiwa unagusa maeneo matatu ambayo ni kuimarisha eneo la ubigwa (udaktari bingwa) kwenye maeneo mbalimbali kama upandikizaji wa figo, moyo na saratani.

Eneo jingine ni ujenzi wa viwanda vya dawa nchini na kuimarisha mifumo ya mawasiliano hospitalini na kuachana na matumizi ya makaratasi kama ilivyo sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles