22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 5, 2024

Contact us: [email protected]

EWURA kuendeleza matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Wadau

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuendana na Mkakati wa Kitaifa unaolenga kuhakikisha Watanzania wanahamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hayo yamebainishwa leo, Julai 5, 2024, jijini Dar es Salaam kwenye maonesho ya 48 ya Kibiashara ya Kimataifa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao katika maonesho hayo.

Kaguo amesema serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika vyombo vya moto, ikiwemo magari, ili kuendeleza matumizi ya nishati safi huku akitoa wito kwa wawekezaji kujikita katika uwekezaji wa vituo vya gesi hiyo – CNG.

“Tunawahamasisha wawekezaji wawekeze kwenye vituo vya ujazaji wa gesi asilia ambapo utaratibu umesharekebishwa na TBS kwamba kituo cha mafuta kinaweza kuwa kinauza gesi asili kwenye magari,” amesema Kaguo.

Amesema EWURA imekusudia kutumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo.

“Kupitia maonesho haya, tumepata fursa ya kukutana na wadau pamoja na wananchi kwa ujumla ili kutoa elimu kuhusu masuala ya petroli, umeme, gesi asilia, pamoja na maji na usafi wa mazingira,” amesema Kaguo.

EWURA inatarajia kwamba kwa kushirikiana na wadau na kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma, matumizi ya nishati safi ya kupikia na gesi asilia katika vyombo vya moto yataleta mabadiliko makubwa katika sekta ya nishati nchini Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles