LONDON, ENGLAND
KIKOSI cha kocha Pep Guardiola, Manchester City, jana kilijikuta katika wakati mgumu baada ya kupokea kichapo takatifu cha mabao 4-0 dhidi ya Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Guardiola anazidi kupaona England pagumu baada ya kichapo hicho ambacho kinazidi kumchelewesha kuingia ‘Top Four’
Everton ambao waliingia uwanjani huku wakitumia mfumo wa 3-4-3, ulionekana kuwafanya waonekane wapo wengi uwanjani kutokana na kuutawala mchezo huo.
Bao la kwanza la Everton liliwekwa wavuni na mshambuliaji wao, Romelu Lukaku, katika dakika ya 34 baada ya kazi nzuri ambayo ilifanywa na Kevin Mirallas.
Manchester City ambao waliingia uwanjani huku wakitumia mfumo wa 4-2-3-1, bado walionekana kuwa na kazi ngumu kuweza kuupita ukuta wa Everton japokuwa mshambuliaji, Sergio Aguero, alishirikiana na Raheem Sterling kujaribu kutafuta bao la kufutia machozi, lakini walishindwa kuonesha uwezo wao.
Baada ya kipindi cha pili kuanza, Everton walionekana kuja kwa kasi kutafuta bao la kuongeza ambapo dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza, waliweza kupata bao ambalo liliwekwa wavuni na Kevin Mirallas baada ya kupokea kazi safi kutoka kwa Ross Barkley.
Hata hivyo, Mirallas baada ya kufunga bao hakuchukua muda mrefu, alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mpya wa timu hiyo ambaye amesajiliwa wiki iliyopita akitokea Man United, Morgan Schneiderlin.
Dakika ya 79, Everton walifanikiwa kupata bao lao la tatu ambalo lilifungwa na mchezaji wao, Tom Davies, kabla ya Ademola Lookman kuongeza bao la nne katika dakika ya 90 na kuzima ndoto za klabu ya Man City.
Kipigo hicho kinamuweka pabaya kocha Guardiola ambaye alipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo ya Ligi Kuu nchini England kutokana na uwezo wake aliouonesha nchini Hispania akiwa na Barcelona na nchini Ujerumani akiwa na Bayern Munich.