24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu usalama barabarani itakavyopunguza vifo kwa wanafunzi

Wanafunzi wakivuka barabara huku wakiwa wameshikana mikono kuepuka kugongwa na magari.
Wanafunzi wakivuka barabara huku wakiwa wameshikana
mikono kuepuka kugongwa na magari.

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

AJALI za barabarani zinazidi kuongezeka kila uchao licha ya kuwapo kwa juhudi mbalimbali za kukabiliana nazo.

Ajali hizo zimesababisha maafa makubwa kwani wako watu waliopoteza maisha, kujeruhiwa, kupoteza mali na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Takwimu mbalimbali zinaonyesha vifo vingi vinatokana na uzembe wa madereva wasiozingatia sheria za usalama barabarani na kusababisha maafa kwa taifa.

Takwimu zilizotolewa wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama, zinaonyesha ajali za barabarani kwa mwaka huu zimeongezeka zaidi tofauti na mwaka jana.

Mathalani kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, takwimu zinaonyesha ajali 4,442 zilitokea kulinganisha na ajali 2,561 zilizotokea kipindi kama hicho mwaka jana.

Kulingana na takwimu hizo, watu 3,127 walijeruhiwa ukilinganisha na watu 2,438 waliojeruhiwa kati ya Januari hadi Septemba mwaka jana.

WANAFUNZI

Vyanzo na tafiti mbalimbali vinaainisha kwamba asilimia zaidi ya 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni abiria na watembea kwa miguu.

Wanafunzi ni kundi mojawapo linaloathiriwa na ajali za barabarani hasa pale wanapokuwa wakivuka barabara kuelekea shule au wakati wa kurudi nyumbani.

Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kwa mwaka jana wanafunzi 78 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani huku 181 wakijeruhiwa.

Kati ya wanafunzi hao wavulana walikuwa 40 na wasichana 78 huku maeneo hatarishi kwa kuongoza kwa ajali hizo yakitajwa kuwa ni Lumumba, Mnazi Mmoja, Mikumi, Mtambani, Boko, Bunju na Kongowe.

ELIMU YA USALAMA BARABARANI

Katika kusaidia kupambana na ajali za barabarani kwa watoto wa shule za msingi na sekondari, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), mwaka jana ilizindua Mpango wa uelimishaji wanafunzi kuhusu umuhimu na sheria za usalalma barabarani kwa wanafunzi ili kuwasaidia kujua sheria za barabarani.

Mpango huo umekuwa ukitoa mafunzo na mbinu zitakazowawezesha wanafunzi kutambua haki zao katika huduma ya usafiri na hivyo kupunguza ajali za barabarani

Mpango huo unaoongozwa na kaulimbiu ya ‘Mtetezi wa haki, masilahi na wajibu wa abiria’ unawawezesha wanafunzi kujumuika pamoja na wenzao na kubadilishana mawazo kuhusiana na changamoto wanazozipata kwenye vyombo vya usafiri na namna ya kuzitatua.

Mpango huo unatekelezwa katika mikoa tisa ambayo ni Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Arusha, Kagera, Kigoma, Mbeya, Mtwara na Tabora na unatarajiwa kuenenzwa katika mikoa yote nchini.

Kupitia mpango huo klabu mbalimbali zimeanzishwa shuleni ikiwa ni mbinu mojawapo iliyobuniwa ili kukabiliana na changamoto ya usafiri kwa wanafunzi.

Hadi sasa vimeanzishwa vilabu 2,300 ambapo katika vilabu hivyo wanafunzi wanapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kupambana na changamoto mbalimbali.

Ikiwa ni sehemu ya uhamamsishaji wanafunzi, wiki iliyopita kulifanyika mashindano ya wanachama wa vilabu hivyo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ya Jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa bajaji na bodaboda wilayani Ilala, Renatus Nicholaus, anasema ili kupunguza  ajali zinazotokea hivi sasa vilabu vya elimu ya usalama barabarani ni muhimu kuanzishwa nchini kote kuanzia shule za msingi ili taifa la kesho liwe lenye vijana makini na watiifu katika sekta ya usafirishaji.

“Kumekuwa na ajali nyingi, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2007, unaonyesha asilimia 76 ya ajali zinazotokea zinatokana na makosa ya kibinadamu yakiwemo ya mwendokasi na uzembe.

“Na ndiyo maana kupitia mpango huu watoto wanawezeshwa kupata elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa usalalma barabarani ili waendelee kuwa mabalozi wazuri miaka ijayo,”anasema Nicholaus.

Akaongeza kuwa kwa upande wa wanafunzi pia wamekuwa wakipata elimu juu ya kukabiliana na unyanyasaji wawapo kwenye vyombo vya usafiri na jinsi ya kuwa watii wa sheria za barabarani.

Utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 16 ya ajali zinasababishwa na ubovu wa miundombinu kama barabara mbaya na kuwa nyembamba.

Shule ya Msingi Msimbazi iliibuka mshindi na kuzawadiwa Sh 100,000 ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Makongo iliyozawadiwa Sh 70,000 na Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa iliyojinyakulia Sh 50,000 ikishika nafasi ya tatu.

Ambapo washiriki walishindana katika kuonyesha sanaa mbalimbali za kuelimisha jamii juu ya usalama barabarani zikiwemo uigizaji, kwaya, ngoma za asili na mashairi.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC), Oscar Kikoyo, anasema walengwa wamekuwa wanafunzi kwa kuwa ndiyo kundi ambalo ni rahisi kuelimika.

“Vijana kama hawa hawana majukumu mengi na ndiyo maana ni wepesi kufundishika, hata tukiwapatia vipeperushi wavisambaze na kuelimisha jamii zinazowazunguka tuna uhakika elimu itafika kwa usahihi na kwa haraka,” anasema Kikoyo.

WALIMU

Kwa upande wake, mmoja wa walimu walezi wa klabu ya Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Masha Sepeku, anasema aina hiyo ya vilabu ni muhimu kwani wanafunzi wanaelimika vya kutosha kuhusu elimu ya usalama wa barabarai na sheria kwa jumla.

Mwalimu Sepeku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu Mkoa wa Dar es Salaam (CCC), anasema kila kilabu huwa na wanafunzi 50 ambapo hufundishwa pia kuwa na kauli nzuri ikitokea kutoelewana na makondata wa daladala.

“Mafunzo ya aina hii yamesaidia sana kwa sababu tangu programu izinduliwe wanafunzi wamekuwa na uelewa na hivyo kupunguza migongano na waendesha vyombo vya moto,”anasema Mwalimu Sepeku.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Kibasila, Mathias Kondrad,anasema uanzishwaji wa vilabu vya aina hiyo shuleni utasaidia wanafunzi kuthaminiwa katika vyombo vya usafiri kama abiria wengine.

“Nimefurahi sana kuanzishwa kwa mpango huu nchini, tuna imani sasa tutathaminiwa kama abiria wengine, tumekuwa tukichelewa shule kwa kukataliwa na hata kupigwa na makondakta ili tusipande magari yao. Lakini sasa hivi tutatumia sheria kudai haki yetu ya msingi kama abiria bila kufanya fujo,” anasema Kondrad.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles