JUMUIYA ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imeziwekea vikwazo nchi za Guinea na Mali, hatua iliyotokana na kikao cha dharura kilichofanyika jana mjini Accra, Ghana.
Uamuzi wa ECOWAS umetokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Guinea hivi karibuni, huku Mali ikiguswa kwa kushindwa kuweka utawala wa Kikatiba tangu jeshi liliposhika dola mwaka jana.
Katika adhabu hiyo, Jumuiya imesitisha msaada wa kifedha, imewawekea kizuizi cha kusafiri viongozi wa jeshi la Guinea waliompindua Rais Alpha Conde, pia ikiwataka kuandaa Uchaguzi Mkuu ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.
Aidha, Ecowas imeitaka Serikali ya mpito ya Mali kutopuuzia makubaliano ya kufanya uchaguzi mkuu ifikapo Februari, mwakani.